Kilolo yaisababishia serikali hasara Sh Milioni 26.7

Wapeleka migogoro ya ndoa Takukuru

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Iringa imeiweka kikaangoni Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh Milioni 26.7, baada ya kushindwa kukusanya mapato hayo yatokanayo na kuhuisha leseni za biashara na ushuru wa huduma.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo leo ya kipindi cha Oktoba hadi Desemba, mwaka jana ; Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Domina Mukama alisema hasara hiyo ni ya kipindi cha mwaka 2021/2022.

“Tulifanya uchambuzi wa ufuatiliaji wa mapato yatokanayo na kuhuisha leseni za biashara na ushuru wa huduma katika halmashauri hiyo na ndipo tulipobaini kuna ufuatiliaji hafifu wa mapato hayo ya serikali,” alisema.

Advertisement

Alisema upungufu wa halmashauri hiyo katika uhuishaji wa leseni za biashara na ushuru wa huduma uliisababishia serikali ikose mapato hayo, ambayo yapo kwa mujibu wa sheria.

Alisema Takukuru imeiagiza halmashauri hiyo kuwafuatilia wote wanaofanya biashara bila kufanya malipo hayo ili walipe, kuhakikisha inatoa elimu kwa walipa kodi ili watimize wajibu na inaimarisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa mapato ya serikali.

Pia Mukama alisema Takukuru ilifuatilia matumizi ya fedha kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Dumilayinga mjini Mafinga wenye thamani ya Sh Milioni 400 na kubaini kuwepo kwa upungufu mkubwa.

Alitaja upungufu huo kuwa ni pamoja na mradi kutekelezwa kwa kasi ndogo, taratibu za manunuzi kutozingatiwa na upotevu wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh Milioni 19.

Baada ya kuingilia kati alisema upungufu huo umerekebishwa, vifaa vilivyoibiwa vimepatikana na watuhumiwa kukamatwa hatua iliyosadia mradi huo kuendelea vizuri.

Pamoja na kuhamasisha sana suala la kuzuia rushwa, Mukama alisema Takukuru bado inapambana na rushwa na kuwachukulia hatua wale wote wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo na katika robo hiyo ya mwaka walipokea malalamiko 44 na kati yake 20 yalihusu rushwa.

Alisema baadhi ya wananchi wameendelea kupeleka malalamiko yasiohusiana na rushwa kama vile migogoro ya ndoa, ardhi na mirathi kwa sababu ya kutofuatilia elimu ya rushwa wanayoitoa kupitia vyombo mbalimbali.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *