HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilwa imepata mafanikio makubwa katika awamu ya tatu ya chanjo ya polio kwa kuchanja watoto zaidi ya 48,761 ikiwa ni asilimia 111.55 ya makadirio ya kuchanja watoto 43,738.
Taarifa hiyo ya ufanisi ilitolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Ruanda Hussein alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mwenendo wa kampeni ya chanjo ya polio wilayani humo.
Alisema wakati wanasubiri awamu ya nne ya chanjo ya polio, wilaya hiyo imefanikiwa katika kampeni ya pili na tatu kwa kuwa walitumia mtindo wa nyumba kwa nyumba wakitumia wataalamu na wahudumu wa afya.
“Awamu ya kwanza ya uchanjaji wa polio haikutuhusu, kwani wenzetu wa mikoa jirani na taifa la Malawi walihusika kwa kuwa tayari Malawi kulikuwa na mgonjwa wa polio lakini awamu ya pili ilikuwa ya kitaifa na hii ya tatu na tumefanya vyema zaidi katika kufikia malengo,” alisema.
Alisema awamu ya pili ya polio ambayo ni ya nchi nzima walilenga watoto 37,864 na kuchanja 43,738 ikiwa ni sawa na asilimia 115 na awamu ya tatu walilengwa 43,738 na kuchanja 48,761 ikiwa sawa na asilimia 111.55.
Aidha, alisema katika kampeni hiyo walikuwa wanakusanya takwimu za ulemavu wa ghafla kwa watoto chini ya miaka mitano na hawakuwapata.
Serikali kupitia Wizara ya Afya iliendesha Kampeni ya Awamu ya Tatu ya kutoa matone ya chanjo ya polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kuanzia Septemba Mosi hadi 4, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio inafanyika kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo uliotokea Malawi, Februari 17 na kisha Msumbiji, Mei mwaka huu.
Ummy alisema kampeni hiyo ya nchi nzima katika awamu ya tatu ya taifa ililenga kufikia watoto 12,386,854 walio chini ya umri wa miaka mitano.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza kuwa unapotokea mlipuko au tishio la mlipuko wa ugonjwa wa polio nchini, nchi husika na nchi jirani zinapaswa kufanya kampeni ya kutoa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa awamu nne mfululizo.
Takwimu za Wizara ya Afya zimeonesha kuwapo kwa mafanikio makubwa katika awamu zilizopita ambazo awamu ya kwanza ya kampeni iliwafikia watoto 1,130,261 sawa na asilimia 115 ya watoto wa umri huo katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma na Njombe ambayo inapakana na nchi ya Malawi.
Katika awamu ya pili iliyofanyika nchi nzima kuanzia Mei 18 hadi 21, mwaka huu, iliwafikia watoto 12,131,049 sawa na asilimia 118.8.
Mwenyekiti Halmashauri ya Kilwa, Farida Kikoleka alishukuru wananchi kwa kuitikia vyema wito wa kuchanja.
Mkazi wa Kilwa Masoko, Fatma Juma alisema kampeni ya nyumba kwa nyumba imeonesha mafanikio makubwa na kutaka iwe inatumika hiyo kila kunapokuwapo na kampeni za chanjo kwani inawafikia mapema.
Mratibu wa chanjo ya Wilaya ya Kilwa, Mohamed Masudi alisema pamoja na kukamilisha siku za kampeni watoto wote ambao hawajafikiwa anashauri wapelekwe kwenye kliniki kwani kampeni ni endelevu.