Kimeeleweka! Simba, Yanga robo fainali CAFCL

CAIRO, Misri: Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba na Yanga leo watafahamu wapinzani wao kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya vilabu Afrika.

Shughuli ya kupanga ratiba ya michuano hiyo itafanyika leo mchana jijini Cairo nchini Misri ambapo macho na masikio ya wapenda soka Tanzania yatakuwa huko kutamani kujua timu zao pendwa zimepangwa na wapinzani gani katika hatua hiyo.

Ikumbukwe Simba na Yanga walimaliza nafasi ya pili katika makundi yao hivyo watakutana na timu zilizomaliza kwenye nafasi ya kwanza.

Advertisement

Wapinzani wa Simba wanaweza kuwa Al Ahly ya Misri, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ama Petro Luanda ya Angola.

Kwa upande wa Yanga mpinzani wake ni kati ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ama Petro Luanda ya Angola.

Tanzania ndio nchi pekee yenye timu mbili katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hii ni kwa mara ya kwanza taifa kupeleka timu mbili katika hatua hiyo.