Kinana akemea rushwa uchaguzi CCM

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Abdulraman Kinana amesema anatamani malaika washuke, ili wajumbe ambao ni wapiga kura wasishawishike kuchukua rushwa.

Akizungumza na wana CCM katika ziara zake mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza, Kinana alionesha kukerwa na vitendo vya rushwa katika chaguzi zinazoendelea na kuzitaka kamati za siasa kutofumbia macho watakaobainika kufanya vitendo hivyo, badala yake wawakate katika kinyang’anyiro cha kugombea.

Akikemea rushwa, Kinana amesema: “Kiongozi anayesaka madaraka kwa nguvu mpaka kutoa hela, huyo hafai kuwa kiongozi, msitafute viongozi kwa umaarufu au fedha zao, kura hazinunuliwi, msikubali kuuza utu wenu, kwa ajili ya pesa.

“Siku zote hawawatambui, hawana habari nanyi, ukifika uchaguzi ndio wanaanza kupitapita na kuwalaghai, natamani malaika awashukie wajumbe, ili msishawishike,” amesema.

Amesema Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ipo wazi kila mwanachama ana haki ya kugombea, kuchaguana na sio kununuliwa.

“Hakuna mwenye hatimiliki ya uongozi, ikiisha miaka mitano mtu yeyote anaweza kugombea, ninyi si ni wajumbe? Kura ni siri, msikubali kuuza kura zenu kwa vipande vya fedha, mtakua mmeuza uhuru wenu, utu wenu, hivyo mtu anayetumia pesa kusaka uongozi msimpe, chagueni kiongozi bora na si bora kiongozi. Mnakubaliana na mimi wajumbe?”Alihoji.

Alisema lazima CCM iwe mfano wa kuigwa katika maadili na jukumu kubwa alilonalo ni kuhakikisha chama kinakua na maadili na uadilifu kwa kuwa chama hicho, ndicho chenye ridhaa ya kuwa sikio la kusikiliza kero za wananchi na kuziwasilisha sehemu husika, zipatiwe ufumbuzi.

“Wananchi wanadhulumiwa tunanyamaza, tusinyamaze, tuwasemee na tuna kazi kubwa ya kusema mazuri yanayofanywa na serikali, niwaombe tumuunge mkono Rais (Samia Suluhu Hassan) na kumtia moyo.

Pia Kinana alikemea tabia ya kuchafuana, ili mwingine ashindwe kugombea na kwamba kamati ya siasa zina taarifa ya kina, watu wasipotoshwe.

“Kuchafuana hapana, kubebana kwa kigezo cha dini, ukabila, ukanda hapana, tafuteni kiongozi kwa haki,” amesisiza

Habari Zifananazo

Back to top button