Kinana aonya wanaomtusi Rais Samia

Asema uvumilivu una mwisho

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amewaonya wapinzani na wale wote wanaotumia lugha za kejeli na matusi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu suala la Bandari kuwa uvumilivu una mwisho.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mkoani Tabora Kinana amesema Rais Samia amekua na mikakati mizuri, kiongozi mtulivu, msikivu, anayepokea ushauri, kiongozi mwenye maono na malengo ambae pia amefungua uhuru mkubwa mno katika nchi yetu.

“Uhuru wa kuishi, uhuru wa kusema, uhuru wa kutoa maoni, uhuru huu sasa unaanza kutumika vibaya.” Amesema Kinana

Akifafanua amesema, Rais Samia alianza mpango wa kukutana na wapinzani nchi nzima kupitia baraza la vyama kuzungumzia hali ya siasa, Demokrasia na namna ya kupata katiba nzuri ambayo inatoa nafasi kwenye uchaguzi kuwa huru na haki ambao vile vile itatoa nafasi ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itatunga sheria ya kusimamia vyama vya siasa lakini Chadema walikataa kuhudhuria.

“Bahati mbaya Chadema walikataa kuhudhuria, hawakwenda kwenye baraza la vyama, hawakwenda kwenye Kituo cha Demokrasia, walikataa.

“Rais mwenye Mamlaka angeweza kusema mmekataa kwa hiyari yenu, wengine wote wamekubali, tunaendelea, hatuwalazimishi, lakini Rais akasema hapana, hawa nao wana hasira, wamekataa kujiunga na wenzao kujadili mambo ya msingi ya nchi yetu, lazima tuwasikilize.

“Alipoamua hivyo, kuna watu ndani ya CCM hata nje ya CCM wa vyama vingine hawakupenda huo uamuzi wa Rais kwa nini awape fursa pekee Chadema, Rais akasema hapana, ngoja niwasikilize kwa nini wamekataa.

“Kwa nini hawataki kushirikiana na vyama vingine, hawataki kushirikiana na serikali na hawataki kunisikiliza mimi, angalia kiwango cha uungwana cha Rais Samia, halazimiki, katiba haimlazimishi, tuliishi hivyo miaka saba iliyopita hakuna mtu aliuliza, ” amesema Kinana na kuongeza

” Rais akasema tukutane akawalika Chadema mwaka jana mwezi wa tano Ikulu Chamwino wakaenda kwenye kikao, upande wa kwanza wa meza walikua viongozi wa CCM, Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msajili wa Vyama vya Siasa na upande wa pili walikaa viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe na mwanasheria wao.

“Kabla ya hapo mtakumbuka Mwenyekiti wa Chadema alikua jela, kabla ya kesi kumalizika Rais akaamua kumualika Ikulu, alipofika alimwambia pole. Hana ulazima wa kumwambia pole lakini ungwana wake umetamalaki.”Amesema

Amesema, mazungumzo ya Rais Samia na Freeman Mbowe yalilenga umoja na mshikamano wakakubaliana kujenga nchi kwa amani na umoja, hatimae mazungumzo ya Chamwino yakazaa matunda, Rais akaamua kuunda kamati ya watu 10, watano CCM na watano Chadema.

“Leo nayasema haya kwa sababu mimi ni Mwenyekiti kwenye kikao hiki kwa upande wa Chama changu na Freeman Mbowe ni Mwenyekiti mwenzangu upande wa pili.

“Walikuja na hoja 15 nyingi ni madai upande wa serikali, CCM hatukua na hata moja. Kwanza kuna wafungwa walikua jela toka kipindi cha uchaguzi walikua 420 waliomba waachiwe, wafungwa wale wameachiwa wote isipokua wawili tu wenye kesi za mauaji ambazo uwezi kuzifuta haraka haraka.

“Sio kwa amri ya Rais lakini DPP aliangalia upya mwenendo wa kesi zao na mashtaka yao wengine walikua wamekataa rufaa, mambo yanafanyika kwa mashauriano na serikali.

“Pili, wakasema wanataka serikali itoe tamko wale wote waliopo nje ya nchi waambiwe warudi na wahakikishiwe usalama wao, mnawafahamu, Tundu Lissu mmoja, Godbless Lema wa pili na Wenje ( Ezekiel), Rais akamuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani (Hamad Masauni) atoe kauli bungeni akatoa. Wamerudi wapo wanafanya shughuli zao za kisiasa hakuna mtu amewagusa.

Kinana anasema, kupitia baraza la vyama vyote vilimuomba Rais kuondoa katazo la mikutano ya adhara na Rais Samia alikubali.

“Angeweza kukataa lakini aliruhusu kwa tahadhari kuwa watu wajenge hoja, waepuke mambo ambayo yatavunja umoja na mshikamano wa Taifa na kuharibu amani.

“Mikutano imeanza tunachosikia sasa
baadhi yao badala ya kujenga hoja wanaleta vihoja, wanasingizia vitu ambavyo havipo, wanasingizia watu uongo, si jambo jema hata kidogo.

” Wanaomtuhumu na kumsema vibaya (Rais) ana Mamlaka makubwa sana, lakini ametulia, amekaa kimya, anavumilia si kwamba hawasikii, anawasikia sana, lakini nadhani ana uvumilivu kuliko wao, ana busara kuliko wao, na anajua Mamlaka aliyonayo akiitumia ipasavyo wataumia.

“Sasa Mimi nataka niwasihi wenzangu, hatukatai mtoe hoja, hatukatai mseme yale mnayotaka kusema, lakini semeni kiungwana, kwa busara, jengeni hoja kusema Rais ana akili za matope, au kusema Rais ameuza bandari wewe sema mkataba huu haujakaa vizuri, toa maoni yako kwa nini haujakaa vizuri.

“Lakini ukisema mkataba huu hata kichaa hawezi kupitisha kwa maana nyingine unatuambia sisi sote vichaa, si sawa hata kidogo.” Amesema Kinana

Amesema, unaweza kupeleka ujumbe mzuri kwa njia ya kistaarabu na ujumbe wako ukaeleweka, lakini pia unaweza kuwa na ujumbe mzuri ukaupeleka kwa kuvurumusha matusi, kejeli na dharau hoja ikapotelea huko

“Watanzania ni wapenda amani, wanapenda kusikiliza hoja, ukishaanza kuvurumusha matusi hoja inaachwa hapo hapo, kwani ni mara ya kwanza kusemwa? alihoji na kuongeza ….; “tangu tumepata uhuru, Hayati Mzee Mkapa kasemwa, JK ( Jakaya Kikwete)kasemwa, marehemu Magufuli kasemwa wananchi bado wapo na CCM. ”

Aidha, Kinana amewasihi watanzania kuimarisha umoja na mshikamano, kuupokee kwa mikono miwili utaratibu huo wa maridhiano na wasiutumie vibaya

“Msifikiri kwa kutukana, kejeli kuonyesha dharau hoja yako itakubalika kwa haraka, hoja itatupiliwa mbali, peleka hoja yako kistarabu itakubalika zaidi.” Amesema

Aidha, Kinana ameonyesha kugadhibiki zaidi kwa kitendo cha baadhi ya viongozi wa Chadema kumtukana Rais Samia wakati amewapatia pesa zao za ruzuku.

“Walikua hawajapokea ruzuku yao, tulipokutana na Rais waliiomba ruzuku na waliomba wapewe yote tangu uchunguzi ulipoisha Rais akasema sawa, andikeni barua, wakaandika wakapewa, , matokeo yake leo wanamuona Rais hana maana, kafungulia mikutano akili za matope, Rais ni binadamu, anahitaji moyo wa uvumilivu sana kuvumilia mambo yote haya, ila kunakuchoka, uvumilivu una mwisho. ” Amesisitiza

Amesema, ajenda zao nyingi walizoomba zimefanyiwa kazi na kuhoji yote anayofanya Rais Samia hastahili kuheshimiwa?

“Kafungua mikutano mnamsakama, hatusemi tunawafanyia hisani ila Rais kawafanyia ungwana sana na nyie kuweni waungwana, jengeni hoja sio vihoja.” Amesisitiza

Awali, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza alisema ifike mahali watu waheshimu Mamlaka ya Rais na kuwaonya wanaopotosha mkataba wa Bandari kuacha mara

“Tusifike mahali tukamdhalilisha Rais na madaraka yake, kuna wanapotosha suala la Bandari, watanzania tuna tabia ya kuamini viongozi wa dini, na viongozi waliopo madarakani, imani hiyo viongozi tusiitumie vibaya kwa kupotosha watu ..

“Hakuna kipengele mkataba ni wa milele, baraza la mawaziri tumeupitia, Kodi itakusanywa na nchi, itaendeshwa kwa sheria za nchi, shughuli zake za uendeshaji hauzidi asilimia nane.”Amesema

Bashe, amesema kuwa wakulima wana maslahi makubwa na bandari kwa kuwa Parachichi ya Njombe ukiisafirisha kupitia km bandari ya Mombasa gharama yake ni Dola za Marekani 9,000 wakati bandari ya Dar es Salaam ni Dola 4,000.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button