MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Bara (CCM) Abdulrahman Kinana ameelezea kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa barabara inayounganisha mikoa ya Kigoma na Kagera.
Akizungumza mjini Biharamulo mara baada ya kuwasili kuanza ziara ya siku mbili mkoani Kagera akitokea Kigoma, Kinana amesema kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ya Kasulu- Nyakanazi si ya kuridhisha.
“ Nimeona kazi inayoendelea ya ujenzi kuna wakandarasi watano na Mungu akipenda itakamilika lakini kuna kuchelewa chelewa kidogo kwa hiyo naomba viongozi wa Kagera, Kigoma na Wizara ya ujenzi kuwasimamia ili kasi iongezeke.” Amesema
Kinana akiambatana na Katibu Mwenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka tayari amewasili mkoani Kagera tayari kwa ziara yake ya siku mbili mkoani humo kukagua miradi mbali mbali pamoja na kukagua uhai wa Chama hicho.