Kinana ataka misaada zaidi waathirika Rufiji

PWANI: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka serikali kuharakisha huduma kwa wananchi wa Rufiji waliopata maafa ya mafuriko, huku uvamizi wa wananchi kwenye eneo la mkondo wa mto na mvua za El Nino zinazoendelea zikitajwa kuwa ni sababu ya mafuriko hayo na si uwepo wa Bwawa la Julius Nyerere.

Hayo yameelezwa leo Aprili 9,2024 katika ziara maalum ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana aliyefika kuwapa salamu za pole waathirika wa mafuriko Rufiji.

Akizungumza na waathirika hao, Kinana amesema sasa hivi maneno mengi hayasaidii, muhimu kuliko yote ni serikali kujihimiza kuwahudumia wananchi, walioathirika.

“Sio wakati wa maneno mengi kinachotakiwa ni huduma ya makazi na chakula, katika hali kama hii ni wajibu wa serikali kuwahudumia wananchi.

“Nimeongea na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kiwango cha huduma kilichotolewa na hali halisi niliyojionea, niseme kasi ya misaada iliyotolewa ni ndogo sana,”amesema.

“Natamani tungepunguza safari za kuja kuona na badala yake tuongeze misaada, watu wanataka makazi, wanataka huduma za afya na wanataka vyakula, tupunguze safari nyingi za watu kuja kuwaona na tukaongeza safari nyingi za watu kutoa misaada…..

“Watu tunawaambia sawa waje lakini kabla hawajaja huduma itangulie. Nimeambiwa yamekuja mahema, blanketi, magodoro na huduma nyingine, lakini idadi ya vitu vilivyoletwa iko mbali sana na mahitaji ya wananchi.

“ Kwa hiyo ni muhimu tukahimiza serikali na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha huduma zinapatikana haraka iwezekanavyo,” amesema Makamu Mwenyekiti Kinana.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Alhaj Abubakari Kunenge amesema kuwa kutokana na mafuriko hayo kuathiri maisha ya wananchi, ombi lao kwa Serikali na Watanzania wote ni kupata misaada ya huduma za kijamii na wao kama Mkoa watahakikisha wanasimamia ugawaji misaada hiyo kwa waliokumbwa na mafuriko hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button