Kinana ataka viongozi CCM kujitambulisha maeneo yao

Kinana ataka viongozi CCM kujitambulisha maeneo yao

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Abdulrahman Kinana, amewahamasisha viongozi wa chama hicho kwa ngazi mbalimbali, kujenga utamaduni wa kuwatembelea na kuwatambua viongozi wa shina, tawi na kata pamoja  na kushiriki vikao vya chama kwenye ngazi hizo.

Kinana ameyasema hayo leo alipokwenda kujitambulisha kwa viongozi wa CCM Tawi la Masaki, pamoja na viongozi wa Kata ya Msasani jijini Dar es Salaam, waliochaguliwa hivi karibuni kupitia uchaguzi wa ndani ya chama unaondelea.

“Nimekuja kuwapongeza, kuwatambua na kujitambulisha kwa viongozi mliochaguliwa katika uchaguzi huu unaondelea ndani ya chama chetu. Nawahimiza viongozi wote kwenda kwenye matawi yao, mabalozi wao, kwenye kata zao, ili wajulikane na washirikiane na matawi yao na viongozi wa matawi na kata. Tunataka viongozi watambue viongozi wanaowaongoza,” alisema Kinana.

Advertisement

Alifafanua yeye ni mwanachama wa tawi na kata hiyo, hivyo anawajibu wa kuwajua viongozi wake kwa sababu kila kiongozi anaye kiongozi mwingine anayemuongoza.

“Nimekuja kutambua viongozi wangu, kwa sababu kila kiongozi ana kiongozi wake anayemuongoza. Makamu Mwenyekiti ana viongozi wake. Unajua kuna watu wanaweza kufikiri Makamu Mwenyekiti hana kiongozi au Mwenyekiti wetu Taifa hana kiongozi, Mwenyekiti wa Taifa ana tawi lake, ana balozi wake.

“Leo hii nimeamua kujitambulisha na kuwatambua viongozi wa tawi na kata, siku nyingine rasmi nitapanga kwenda kuonana na wanachama wenzangu na kwenda kutambua balozi wangu,” alisema Kinana alipokuwa akijitambulisha, mimi ni mwanachama wa kata hii nina wajibu wa kuwajua viongozi wangu.

“Nilikuwa nawaambia wenzenu pale kwenye tawi kwamba CCM imesimama kwenye miguu miwili, mguu wa kwanza ni wanachama, msingekuwa hapa bila wanachama, msingekuwa kwenye uongozi wa nchi bila wanachama, tusingepewa ridhaa ya kuongoza nchi hii bila wanachama, kwa hiyo wenye dhamana kubwa wanachama wenu, wanastahili heshima zote na kuthaminiwa,” alisema na kuongeza:

“Ningependa kusisitiza viongozi kila wakati tukumbuke wanachama wetu, kuna hatari unapokuwa kiongozi unapoona nafasi uliyonayo umeipata kwa akili yako, busara zako na kwa uwezo wako na maarifa yako sio kweli. Unaweza kuwa na sifa zote, lakini wanachama wakisema hapana huwezi kuwa kiongozi, kwa hiyo wakati wote tutambue thamani ya wanachama wetu.”

Akifafanua zaidi Kinana alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimesimama kwenye miguu miwili ambayo ni wanachama na Katiba.

“Viongozi wanatokana na wanachama kwa hiyo lazima tuwaheshimu, tuwatukuze na tuwafuate. Kwa bahati mbaya siku hizi kumekuwa na utamaduni wa viongozi wa CCM wanaitwa mheshimiwa, lakini ukweli sisi wote ni ndugu. Ndugu Mwenyekiti na ndugu Rais, lakini imefika hatua hata balozi anaitwa Mheshimiwa Balozi, ukiitwa mheshimiwa unakuwa mbali na watu na ukiwa ndugu unakuwa karibu na watu,” alisema.

Kinana alisema nguvu ya pili ya chama inatokana na Katiba huku akifafanua pamoja na uwepo wa katiba nzuri bado wanachama wanayo nafasi kubwa.

Aliwakumbusha viongozi wa Kata ya Msasani kumwandikia barua zinazohusu vikao vya kata na kuahidi atashiriki na iwapo atakuwa na udhuru atatoa taarifa.

“Mkiandika barua ya kunihitaji kwenye vikao vya Chama chetu ngazi ya tawi, kata nitakuja.”