Kinana: Hakuna mfumo mzuri wa kuwatambua wazee

GEITA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema kama taifa hakuna mfumo mzuri wa kuwatambua wazee.

Kinana ameyasema hayo katika ziara yake mkoani Kagera na Geita na kudai kuwa kitendo cha kutokua na mfumo sahihi na madhubuti ndicho kinasababisha wazee kutofikiwa kwa ukaribu na kupata huduma stahiki ikiwemo matibabu.

Akizungumza na wazee hao amesema, “wazee sio kwamba tumewasahau hata orodha ya nyinyi hatuna, hatuwafahamu, nadhani ni wajibu viongozi wa Chama kuwakumbusha watendaji wa Mitaa kuwa na orodha ya wazee, “amesema Kinana na kuongeza.

“Wakati mwingine anafariki Mzee ambae alikua kada maarufu lakini viongozi wa sasa wa Chama hawafiki kwenye msiba kwa nini, kwa sababu hawamjui, na hiyo yote ni kwa kuwa hatuna mfumo sahihi wa kuwatambua, “amesema.

Aidha, amesema ni wakati wa chama cha CCM kujikosoa na kujisahihisha.

“Hayati Mwalimu Nyerere hata kwenye kitabu chake ameandika tujisahihishe, chama kizuri ni kile kinachokubali makosa, tukisema CCM hatukosei kabisa sio kweli, tujisahihishe ili tujihimarishe. ” amesema.

Awali, wakielezea changamoto zao wazee hao walimueleza Kinana kuwa bado wanapokwenda kupata huduma za afya wanakutana na vikwazo katika kupata hudumu ikiwemo kutokuwa na uhakika wa kupata matibabu ya uhakika.

Sylvano Kayoza amesema iwapo wazee watawekewa utaratibu mzuri wa matibabu wakawa na uhakika wa kutibiwa kila wanapohitaji itawaongezea fursa ya kuishi kwa furaha kwa muda mrefu.

Amesema ingawa hivi sasa wamewekewa dirisha maalumu la kupatiwa huduma hususan katika hospitali ya wilaya na mkoa, lakini bado wanakumbana na changamoto ikiwemo ya kutakiwa kununua dawa kwa gharama zao nje ya hospitali kwa kuwa hazipatikani hospitalini.

Kwa upande wake, Maulid Kambuga aliipongeza serikali kwa kutekeleza mambo yenye maslahi ya wengi.

Haya hivyo aliiomba serikali kutowachekea watu wachache wenye nia mbaya ya kukwamisha maendeleo kutokana na ubinafsi.

Kinana amehitimisha ziara yake katika mikoa ya Kagera na Geita baada ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na uhai wa chama hicho.

Habari Zifananazo

Back to top button