GEITA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulurhaman Kinana amesema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi nzuri na wakati mwingine anasikia zimeanza kauli mbona mnamsifu sana huyo Rais.
“Nasikia, kila kitu Rais Rais Rais, lakini lazima tukubaliane baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema hivi kuongoza ni kuonesha njia , ukiwa na kiongozi mzuri , msikivu, mwenye kushirikiana na wenzake wakapanga na mambo yakawa kwa nini tusimsifu , lazima tumsifu maana ndio anatuongoza, ” amesema Kinana.
Kinana ameyasema hayo leo Desemba 12, 2023 katika Mkutano wa wananchi wa Jimbo la Chato mkoani Geita, ambapo amesema miaka ya nyuma Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, walikua walisema zidumu fikra za Mwenyekiti.
“Lakini fikra hazikuwa za Mwenyekiti ni za chama cha TANU na CCM, kwa sababu gani? Ndio kiongozi wetu anafanya kazi nzuri , Rais Samia kwa muda mfupi sana amefanya kazi kubwa sana.
“Ukimwambia Mkuu wa Mkoa hapa (Martine Shigela) asimame aeleze fedha zilizoletwa katika Mkoa huu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, basi nina hakika fedha zinazotolewa kipindi cha Rais Samia inaweza kuwa mara 10.
“Nilikuwa Kagera wamepewa fedha Sh bilioni 260, nilikuwa Rukwa wamepewa Sh bilioni 256 Mkuu wa Mkoa Geita, ananiambia zaidi ya Sh bilioni 300 zimeletwa kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesema.