Kinana: Kataeni kufarakanishwa

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana

DODOMA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekemea vikali ubaguzi wa Uzanzibari na Uzanzibara unaoendelea na kudai kuwa Muungano katu hautavunjika kwani ni wa mfano wa kuigwa duniani.

Chama hicho pia kimetaka Watanzania kutokubali kufarakanishwa, kupandikizwa chuki dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hana nia njema na Bara.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza na Wananchi, mkoani Dodoma katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete

Akizungumza na Wananchi wa Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana amesema muungano uliopo umepitia kashikashi nyingi, majaribu mengi lakini bado umeendelea kuwepo, waasisi wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Karume walijenge msingi imara na leo tunaazimisha miaka 60 ya Muungano hivyo hakuna atakayeuvunja muungano huo.

Advertisement

“Kilichofanya Muungano huu ukadumu ni historia, Bara na Visiwani tuna historia moja, utamaduni, lugha, undugu na mapambano wakati TANU NA ASP vinapambana vyama vilishikamana kukomboa nchi zetu, hakuna atakayetufarakanisha,”amesema Kinana.

Amesema hoja za upinzani ni kwamba Zanzibar ni ndogo sana wanakuaje na wabunge wengi wakati wao ni milioni 1.

4 pili wanasema Rais Samia Mzanzibar hana nia njema na sisi na kwamba maneno hayo hayana ukweli hata kidogo.


“Rais kaingia madarakani kwa katiba ya Tanzania amekula kiapo eti ana dhamira mbaya na upande wa pili wa muungano uongo ukirudiwa rudiwa usiposahihishwa itafanywa kuwa kweli, watanzania kataeni sumu inayopandikizwa mioyoni mwenu.

“Baba wa taifa angesema tuimeze Zanzibar sasa hivi tungekuwa tunagombana, aliona mbali, Karume alitaka nchi iwe moja.

Chadema wanataka kutufarakanisha, kutukoroga, nchi imetulia wanataka watanzania kutugawanya msikubali, tusikubali.

Tupo tayari kukosolewa na kikundi chochote, lakini hatupo tayari kukubali umoja wa kitaifa ukavurugwa,”amesema.

Amesema, CHADEMA wanakuja na hoja anateuliwa Mkuu wa Mkoa anapelekwa mkoa ambao si kwao, anateuliwa Mkuu wa wilaya wanasema mkoa aliopelekwa sio kwao.

“Kwa hiyo tunaanza mambo ya kwao na kwetu, itafika mahali watu watasema umekuja kufanya biashara kwangu ondoka ndicho tunachotaka?

Hapana, ndiko tunakopelekwa na wapinzani,”amesema Kinana.

Amesema Rais Samia ana nia na dhamira ya dhati na Bara, hoja za wapinzani kuwa hana huruma na Bara, hana jema analolitakia upande wa Bara, hana msaada kwa watu wa Bara, ni hoja mfu na kwamba wanataka kumdhalilisha, kumtenga Rais Samia na watanzania.


“Rais Mzanzibari…. Rais Mzanzibari…. Nani kakataa Rais Samia kuwa sio mzanzibari katoka Zanzibar katiba inasema mgombea akitoka upande wa Muungano mgombea mwenza atatoka upande wa pili ndivyo tulivyokubaliana, kitu gani cha ajabu na mgombea mwenza ana umuhimu sawa sawa na mgombea

“Chadema wanatafuta namna ya kutuvuruga wameangalia huduma za jamii zinakwenda vizuri, maji, barabara, elimu, afya makao makuu Dodoma yanajengwa, bwawa la umeme linafanyiwa kazi, wakaona hawana pa kutokea, tujenge hoja Mzinzibari, hatufai, Rais huyu ni Rais wa katiba alikuwa mgombea mwenza kwa msingi wa katiba, alirithi baada ya Magufuli kufariki na alirithi kikatiba hakwenda mwenyewe,” amesema Kinana.