Kinana: Muwe wakali kuisimamia serikali

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amewataka wabunge na madiwani wa chama hicho wawe wakali katika kuisimamia serikali ili itekeleze ahadi za miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Kinana alitoa agizo hilo jana katika kikao cha ndani kilichofanyika katika ofisi ya chama hicho mkoani Geita.

Kinana alisema kuna baadhi ya miradi ikiwemo ya maendeleo ambayo inatengewa fedha nyingi lakini fedha hizo zinaelekezwa sehemu nyingine.

“Mimi ni mmoja wa watu ambaye ninapenda wabunge wawe wakali kidogo kuhusu mambo ya serikali. Sio wakali kwa maana ya kuisakama Serikali lakini wawe wakali kwa kuiwajibisha serikali,” alisema Kinana na akaongeza;

“Unajua hiki chama ndicho kinachokwenda kwenye uchaguzi, hiki chama ndicho kinachoomba kura, hiki chama ndicho kitakachopewa viongozi au kitakachonyimwa sio Serikali.”

Kinana alisema iwapo mambo hayatakwenda vizuri kitaadhibiwa chama na si vinginevyo na akasema kwenye mambo ya wananchi lazima viongozi hao wawe wakali.

Alisema kila mmoja kwenye nafasi yake atimize wajibu wake ikiwa ni pamoja na kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kufanikisha malengo ya kuwatumikia wananchi.

Kinana alisema Bunge, kamati za bunge, halmashauri, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na mawaziri wanapaswa kutimiza wajibu wao.

“Rais anajitahidi sana lakini Rais hayuko peke yake. Rais ni taasisi. Nchi hii si mali yake na katika uongozi lazima atumie taasisi, atumie taratibu, kanuni, sheria pamoja na sera na sisi wote tumsaidie Rais ili aweze kufanikiwa. Mmesema hapa (Geita) Rais ametoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo,” alisema.

Kinana alisema katika ziara zake mikoani amekuta miradi inasuasua kwa sababu ya fedha zilitengwa halafu hazipo.

“Nilikuwa huko Rukwa, Katavi na sasa hapa. habari ndio hiyo hiyo, hata kama huna uwezo wa kutoa fedha zote basi toa kiasi fulani halafu tujue kwamba umeshindwa lakini uwaambie fedha hizi ilikuwa tutoe lakini zimekwenda mahali pengine, hilo sio jambo jema sana,” alisema.

Aidha, Kinana alikerwa na migogoro ya ardhi inayoendelea katika mikoa mbalimbali ikiwemo Geita.

“Mkuu wa Mkoa wa Geita jana na leo tumezungumza, nadhani hili jambo ni muhimu sana na lazima ifike mahali liishe. Nchi hii ina migogoro mingi sana ya ardhi, kila mahali ardhi ardhi. Juzi nilikuwa Kigoma tulifanya mkutano kuanzia saa tisa mpaka saa 2:30 usiku na wana CCM,” alisema Kinana.

Aliongeza: “Nusu ya muda tumezungumzia ardhi na mgomvi mkubwa ni ardhi… ardhi, ardhi, ardhi. Sasa lazima tufike mahali tupate ufumbuzi. Hapa kwenu (Geita) mna matatizo na misitu, mgororo kati ya wananchi na misitu , mgororo kati ya wananchi na hifadhi. Mgogoro huu sio wa leo,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button