MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amesema Hayati Mwalimu Julius Nyerere ataendelea kuwa kielelezo kizuri cha Taifa la Tanzania, shule ya uongozi, darasa la uadilifu na mfano wa kila jambo katika Tanzania.
Pia, ni shujaa namba moja ambae aliliongoza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kumuondoa Nduli Idd Amin mwaka 1978.
Kinana, ameyasema hayo leo Julai 25, 2023 alipozuru kaburi la Mwalimu Nyerere Mwitongo Mara na kuweka shada la maua na baadae kwenda kumjulia hali Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali David Musuguri na kumpa zawadi.
Kinana amesema, vita ya Kagera ilikuwa fupi sana na haijawahi kutokea duniani.
“Wanajeshi wa Tanzania walimaliza kazi ile kipindi kifupi sana, vita ya Nduli ilianza mwezi wa 11 mwaka 1978 kuikomboa eneo la Tanzania.
“Wanajeshi wetu walipigana kwa ujasiri, ushujaa, ufanisi kutoka mto Kagera hadi Mpaka wa Uganda na Sudani ya Kusini. “Amesema Kinana na kuongeza
” Mashujaa walimwaga damu kwa ajili ya nchi yetu, na walimwaga damu kwa ajili ya Bara la Afrika, nina hakika kila Mtanzania anakubali shujaa namba moja ni mwalimu Nyerere, aliongoza majeshi yetu akiwa Amir Jeshi Mkuu, kwa kufanya kazi ya kumng’oa Idd Amin, aliongoza ukombozi wa bara la Afrika nzima.
“Alisimamia haki na usawa duniani, ni baba wa taifa anayeheshimika nchini na ataendelea kuheshimika, kumuenzi, anathaminiwa katika bara hili, kila mtu anafahamu mchango wake na kazi yake kubwa aliyoifanya,dunia inatambua.”Amesema
Vita ya Kagera ilianza mwaka 1978 hadi Aprili 11 1979 katika mkoa wa Kagera unaopakana Kaskazini magharibi mwa nchi ya Tanzania ambapo Majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana Majeshi ya waasi Uganda yalimuondoa kiongozi wa kijeshi wa wakati huo nchini Uganda Idd Amin Dada.
Aidha, Kinana amesema jambo moja ambalo baba wa Taifa ataendelea kukumbukwa nalo ni jeshi la Tanzania halikwenda kuikalia Uganda, baada ya kumaliza kazi ile walirejea nyumbani
“Sitaki kuzitaja ila kuna nchi ambazo zilivamia nchi nyingine, zikakaa miaka 10, miaka 20 zikaondoka kwa aibu, haikutokea kwa nchi yetu, majeshi yetu chini ya baba wa taifa walifanya kazi waliopewa kufanya walipomaliza akawaagiza rudini nyumbani haraka na jeshi likarudi nyumbani kwa heshima kubwa; ……..”Mpaka leo Uganda chini ya Rais Yower Museven wanamuheshimu baba wa taifa, wanaheshimu kanuni ya baba wa taifa, wanaheshimu taifa letu na uhusiano mzuri. ” Amesema
Comments are closed.