Kinana: Uongo ukisemwa sana unaaminika

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahaman Kinana akizungumza na Wananchi wa Dodoma kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete

DODOMA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahaman Kinana amesema, siku za karibuni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa kikizunguka na kufanya maandamano kutuhuma CCM na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Dodoma, kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete leo Mei 5, 2024, Kinana amewatuhumu CHADEMA kwa kusema uongo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahaman Kinana akizungumza na Wananchi wa Dodoma

“Hatukatai kukosolewa wala kusahihishwa ila sio kwa mambo ya uongo ambayo hayapo, nataka kutumia jukwaa hili kueleza msimamo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kauli za uongo za CHADEMA,

Advertisement

“kuna mtu mmoja Mjerumani wakati wa enzi za Hitler, huyo mtu alikuwa maarufu sana wa kuzusha mambo, wa kutengeneza uongo, na ana kanuni ameitengeneza, kanuni hiyo inasema hivi: ‘tengeneza uongo, urudie mara kwa mara mpaka watu wauamini huo uwongo’ na hicho ndicho wanachofanya ndugu zangu wa CHADEMA,

“Kazi yao ni kusema uwongo, lakini uwongo huo wanaurudia kila wakati ili Watanzania wauamini , kwenye hilo sina shaka hata kidogo kwamba Watanzania hawauamini uwongo wao hata kidogo, na kanuni hiyo wanayokwendanayo, ya kutengeneza na kusambaza uwongo dhidi ya CCM, serikali ya CCM na Rais wake watashindwanayo,”ametuhumu Kinana.