Kiongozi mbio za mwenge ataka zahanati kukamilika kwa wakati

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalah Shaib Kaim ametaka mradi wa zahanati unaojengwa kwa gharama ya Sh milioni 100.9 katika kijiji cha Kwemakame,wilayani Lushoto mkoani Tanga kukamilika kwa wakati.

Akiongea wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembele zahanati hiyo na kuweka Jiwe la Msingi, Kaim alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mradi huo na kutoa rai kwa wasimamizi kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili kuwapunguzia wananchi adha ya huduma ya afya .

“Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika sekta mbalimbali miradi ya maendeleo ikiwemo ya afya tunamshukuru sana Rais wetu mama Samia ,tunachohitaji ni kuona mradi huu unakamilika kwa wakati  na wananchi wanapata huduma stahiki.” amesema Kaim.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi huo, zahanati hiyo ilianza kujengwa mwaka 2017 kupitia nguvu za wananchi ,mapato ya ndani ya halmashauri ,mfuko wa jimbo na wahisani na unatarajiwa kukamilika ifikapo juni mwaka huu kwa thamani ya Sh milioni 100.93.

Naye Mbunge wa Jimbo la Lushoto, Shaban Shekilindi alisema ujenzi wa zahanati hiyo ni utekelezaji wa mipango ya selikali katika kuwasogezea karibu huduma za afya wananchi wake.

Alisema kabla ya zahanati hiyo wananchi wake walikuwa wakitembea umbali wa km 14 hadi 24 kufuata huduma ya matibabu jambo ambalo lilikuwa linafifisha juhudi za serikali kusogeza karibu huduma za afya.

“Serikali imeahidi kutoa sh, milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha zahanati ila tunaomba ikiwezekana tuletewe haraka watumishi na tunataka zahanati hii iwe kituo cha afya iweze kuhudumia wananchi wengi zaidi”

Wakati huohuo,Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la Msingi mradi wa kituo binafsi cha mafuta cha Perango kilichopo kata za Lushoto na Lukozi kinachogharimu kiasi cha Sh milioni 240.

Mkurugenzi wa kituo hicho cha Mafuta, Peter Ngowi alisema ujenzi wa kitu hicho umeleta  manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo kwa kuwasogezea karibu huduma ya maji safi ya kunywa wanayochota bure pamoja na ajira kwa vijana wasiopungua 10 .

“Mradi huu umeleta hamasa kubwa ya uwekezaji kwa sekta zingine zinazotumia mafuta kama nyenzo ya uendeshaji kuja kuwekeza katika maeneo  hayo jambo ambalo litasaidia kuvuta maendeleo katika kata hizo”

Aidha alisema mpango wake ni kuendelea kufungua vituo vingine vidogo vya mafuta ili kuwasogezea huduma hiyo wananchi wanaoishi umbali mrefu na hivyo kuchochea uchumi wa wakazi wa Lushoto na viunga vyake.

Habari Zifananazo

Back to top button