MAHAKAMA nchini Zimbabwe imemhukumu kiongozi wa upinzani, Tendai Biti kifungo cha miezi sita jela au faini ya Dola 300 kwa kumshambulia kwa maneno mfanyabiashara wa Urusi.
Hakimu Vongai Guwuriro aliamua kwamba Tendai Biti, waziri wa zamani wa fedha wa Zimbabwe, lazima alipe faini hiyo au afungwe, na hivyo kumaliza vita vya kisheria vilivyodumu kwa miaka minne kati ya Biti na Tatiana Aleshina ambaye alikuwa mwekezaji wa urusi.
Alec Muchadehama, wakili wa Biti, aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama ya Harare Jumanne kwamba Biti atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
“Mimi na Tendai Biti tumesikitishwa sana na hukumu hiyo, lakini sishangai,” alisema. “Ndio maana tunaenda kukata rufaa Mahakama Kuu, tunazo sababu mbalimbali ambazo tutazieleza katika misingi yetu ya rufaa.
”
Waendesha mashtaka wa serikali walimshtumu Biti kwa kumwita Aleshina “mpumbavu” na kumnyooshea kidole mwaka wa 2020. Biti alikanusha shtaka la kumshambulia kwa maneno.
“Zimbabwe imepata haki, hata kama imechukua muda wa miaka minne. Lakini nilijifunza mengi. Niligundua kama sisi wanawake hatuwezi kutetea haki zetu, haki haitadhihirika,” alisema. “Na sina uhusiano wowote na Tendai Biti, au mtu yeyote, lakini ajifunze kuheshimu wanawake, na kuheshimu sio wanawake tu, bali kila mtu katika nchi hii.” Aleshina alisema uamuzi huo ni ushindi kwa wanawake.