SERIKALI ya Somalia inasema imemuua Abdullahi Nadir, mmoja wa waanzilishi wa kundi la al-Shabab, katika operesheni na washirika wa kimataifa.
Wizara ya habari ya nchi hiyo ilisema katika taarifa yake Jumapili kwamba operesheni iliyomuua Nadir ilifanyika Jumamosi. Ilisema alikuwa mwendesha mashtaka mkuu wa al-Shabab na alikuwa katika mstari wa kuchukua nafasi ya kiongozi wa kundi hilo, Ahmed Diriye, ambaye ni mgonjwa.
“Kifo chake ni mwiba ulioondolewa kutoka kwa taifa la Somalia,” taarifa hiyo ilisema. “Serikali inawashukuru watu wa Somalia na marafiki wa kimataifa ambao ushirikiano wao uliwezesha kuuawa kwa kiongozi huyu ambaye alikuwa adui wa taifa la Somalia.”
Katika wiki za hivi karibuni, vikosi vya usalama vya Somalia vimepongeza mafanikio yaliyopatikana dhidi ya kundi lenye uhusiano na al-Qaeda wakati wakipigana pamoja na vikundi vya kujilinda vya ndani. Lakini al-Shabab wameendelea kufanya mashambulizi mabaya, ikiwa ni pamoja na mawili ya Ijumaa iliyopita ambayo yaliwauwa takriban watu 16.
Tangu mwaka 2006, kundi hilo limeua makumi ya maelfu ya watu katika mashambulizi ya mabomu katika vita vyake vya kupindua serikali kuu ya Somalia inayoungwa mkono na Magharibi na kutekeleza tafsiri yake ya sheria za Kiislamu.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, aliyechaguliwa na wabunge mwezi Mei, ameahidi kupeleka vita kwa waasi baada ya miaka mitatu ambapo mtangulizi wake, aliyekumbwa na vita vya kisiasa, alichukua hatua kidogo dhidi ya al-Shabab. Mwezi Agosti, Mohamud alimteua msemaji wa zamani wa al-Shabab Muktar Robow katika baraza lake jipya la mawaziri.