Trending

Kishikwambi kilichoporwa kwa karani wa sensa Katavi chapatikana

KISHIKWAMBI cha karani wa sensa kilichoibwa usiku wa Agosti 23 huko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi kimepatika, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amethibitisha.

Mrindoko amesema licha ya Karani huyo kupoteza kifaa chake cha kazi zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 halikuteteleka na kwamba limeendelea vizuri.

“Tulifanya msako na Kishikwambi kilipatikana mchana ule,” amesema RC Mrindoko. “Kwa hiyo hakukuwa na athari zozote kwenye zoezi la sensa kwa sababu tayari alipatiwa kishikwambi kingine, na hata kabla ya kuanza kukitumia kifaa chake cha awali kilipatikana.”

Ameongeza kuwa vifaa vya mazoezi ya kiserikali hutokana na kodi za wananchi hivyo vinapaswa kulindwa, na endapo watakuta karani anafanyiwa kitu au kuwa na dalili za kifaa kupotezwa wananchi wanapaswa kumsaidia karani.

“Niwaombe wananchi tuendelee kudumisha usalama wakati wa kuhesabiwa yaani makarani wale na vifaa vyao vyote walivyonavyo, wakiwa nyumbani au kazini tusaidiane kuhakikisha makarani wanakuwa salama na vifaa vinakuwa salama ili tuweze kufanikisha zoezi hili kwa ufanisi wa asilimia mia moja”.

Hata hivyo amesema mpaka sasa zoezi la sensa katika Mkoa huo linaendelea vizuri na kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kushiriki zoezi hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button