Kiswahili ‘dili’ nje ya nchi

Jumla ya balozi 13 zimenzisha madarasa, vituo na klabu za za Kiswahili nje ya nchi, Bunge limefamishwa leo Jumatatu, Mei 22, 2023.

Kufunguliwa kwa vituo hivyo, jumla ya Watanzania 95 wamepata ajira katika maeneo hayo.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Ameir Abdallah Ameir aliyetaka kujua namna Balozi zinavyotumia fursa ya kukua kwa lugha ya Kiswahili nje ya nchi.

Mbali na fursa hizo, Naibu Waziri ameongeza, vyuo na vituo binafsi zaidi ya 150 vinafundisha Kiswahili duniani.
“Kwa sasa, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limepewa kazi ya kufundisha walimu kumi (10) wa Diaspora katika Ubalozi wetu wa Abu Dhabi ambao ulihitaji walimu wa kwenda kufundisha Kiswahili katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

“Mheshimiwa Spika, baadhi ya Balozi zetu zipo katika mazungumzo na vyuo vikuu kwenye maeneo yao ya uwakilishi ili lugha ya Kiswahili iweze kujumuishwa katika mitaala ya vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kupata wahadhiri wa Kiswahili kutoka Tanzania,” ameongeza.

Miongoni mwa vyuo hiyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kuwait, Chuo Kikuu cha Holon Institute of Technology nchini Israel na Chuo Kikuu cha Buraimi nchini Oman.

Katika utangulizi wa majibu yake, Geofrey amesema, Wizara kupitia Balozi zetu nje ya nchi zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali katika kukuza Kiswahili na kuchangia ongezeko la ajira kwa Watanzania.

Ameeleza kuwa programu hizo zinajumuisha kufundisha, kutafsiri na kufanya ukalimani wa Kiswahili duniani, hatua ambayo inatoa ajira kwa Watanzania.

Habari Zifananazo

Back to top button