Kiswahili kufundishwa Uswisi
SERIKALI imepeleka wataalam wa Lugha ya Kiswahili kutoka Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na Baraza la Kiswahili la Kiswahili Zanzibar (Bakiza) Geneva nchini Uswisi kufundisha Kiswahili kwa wana Diaspora.
Katika mafunzo hayo jumla ya wanadiaspora 15 wamejiunga na darasa hilo na watakapofuzu mafunzo hayo ya wiki moja, watakuwa wakufunzi na walimu wa kiswahili kwa wanafunzi nchini Uswisi.
Naibu Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Hoyce Temu amesema Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na watu wengi duniani na kwa kutambua hilo, Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) lilitangaza Julai 7 kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili Duniani.
“Kufundishwa kiswahili Geneva ni fursa, siyo tu kuitangaza Tanzania na nchi zinazozungumza Kiswahili bali pia kukifanya Kiswahili kuwa kama bidhaa,” amesema Hoyce na kuongeza
“Watanzania tuchangamke, kuna fursa mbalimbali zikiwemo ukalimani, tafsiri, uandishi wa vitabu na katika vyombo vya habari,” amesema.