Kiswahili kuongeza ufafanuzi wa sheria

Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kutafsiri sheria za Tanzania yataongeza uelewa kwa wananchi ambao utasaidia kujua haki na wajibu wao katika utatuzi wa migogoro mbalimbali inayowakabili.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Griffin Mwakapeje amesema hayo wakati akitoa wasilisho kuhusu mchango wa lugha ya kiswahili katika upatikanaji wa haki.

Amesema matumizi ya lugha ya kingereza badala ya lugha ya kiswahili kinachoeleweka na kutumiwa na wananchi
wengi inawanyima kufahamu na kuelewa sheria mbalimbali.

Hivyo Mwakapeje ameliomba Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuendelea na utafiti ili kupata misamiati muhimu itakayotumika katika sheria ili kuwaondolea ukakasi mahakimu na majaji kwa kuwa wanapata ugumu katika kuandika hukumu kwa lugha ya Kiswahili.

Pia amesema kwa sasa Tume ya Kurekebisha Sheria ipo katika utekelezaji wa jukumu la kutafsiri sheria na ripoti mbalimbali za kisheria kutoka lugha ya kingereza kwenda lugha ya Kiswahili.

“ Sisi tunapokwenda kutoa elimu kwa wananchi tunaona hitaji la sheria na machapisho mbalimbali kuwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwasaida kufanya rejea mbalimbali;” amesema.

Amesema Tanzania ina jumla ya sheria 550 ambapo kati ya hizo zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ni 246 ambapo bado juhudi zinaendelea kukamilisha kazi hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button