TANGA: Naibu Waziri wa maliasili na utalii, Dastun Kitandula anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya Magamba Walkthon and Adventure.
Mashindano hayo yatafanyika Desemba 17, 2023 katika hifadhi ya msitu wa asili wa Magamba iliyopo wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalist Lazaro amesema kuwa mashindano hayo yana lengo la kutangaza fursa za utalii zilizopo kwenye hifadhi hiyo na wilaya kwa ujumla.
“Tunakwenda kuifungua Lushoto kupitia mashindano hayo kwa kuhamasisha Watanzania kupenda kutembelea vivutio vya nchini mwao badala ya kutegemea wageni pekee”amesema DC Lazaro.
Nae Mhifadhi Mwandamizi wa hifadhi ya msitu wa asili wa Magamba, Christoguns John amesema kuwa mashindano hayo yatahusisha mashindano ya kutembea na baiskeli.
“Tayari zaidi ya washiriki 150 wamejitokeza kushiriki kwenye mashindano hayo yatakayohusisha matembezi ya Km 5,10 na 15 huku baiskeli ikiwa ni Km30″amesema John.