Kitandula: pandeni miti kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii,Dunstan Kitandula ameagiza watanzania kupanda miti pale wanapoikata ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kipindi hiki ambacho ulimwengu hauko salama.
Kitandula ameagiza hayo wakati akifunga kongamano la pili la Kimataifa la Viongozi Vijana la Mabadiliko ya Tabia Nchi lililofanyika mkoani Dar es Salaam na kukutanisha vijana zaidi ya 200 kutoka nch 24 duniani.
Amesema mabadiliko ya tabianchi ni jambo halisi hivi sasa ulimwenguni kote ambayo kwa kiasi kikubwa yamesababishwa na shughuli za kibinadamu katika kuharibu mazingira.
“Serikali imefanya kazi kubwa ya kuwa na mipango ya kupambana na tatizo hili.
“Inawezekana katika kupeana majukumu haya ya kupanda miti pengine hatujayasimamia vizuri kwamba wale tunaopewa jukumu la kupanda miti tukishapanda tunafuatilia kuhakikisha miti hiyo inaota na inakua,” amesema.
Amepongeza kongamano hilo kwa kuunga jitihada za serikali kwa kupanda miti aina ya mikoko eneo la ukanda wa bahari kwa kuwa miti hiyo ina kiwango kikubwa cha kupanbana na hewa ya ukaa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania ( TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema vijana hao kutoka nchi 24 duniani wamekua na kongamano la siku nne kupaza sauti na kujengeana uwezo wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi duniani.
Naye Mwana sayansi wa mazingira Shamim Nyanda amesema katika kongamano hilo wamejifunza baadhi ya vitu kutoka kwa vijana wenzao katika nchi 24 ambavyo watavifanyia kazi ikiwemo kushirikiana na serikali kupitia wizara ya mazingira.