GEITA: MRADI wa Zahanati ya Budoda wilayani Mbogwe ulikwama kwa miaka 18 sasa unaenda kukamilika baada ya serikali kutenga zaidi ya Sh milioni 50.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Jacob Julius (JAJU) amewahakikishia wananchi wa Kijiji hiko kuwa Zahanati hiyo imeshatengewa bajeti kwa mwaka huu wa fedha 2023.
Jacob amewahakikishia wananchi hao nia njema ya Rais, Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwapa maendeleo watanzania kwa usawa bila ubaguzi.
“Mkuu wa Wilaya yetu Sakina Jumanne ndiye msimamizi mkuu wa Wilaya yetu, mwenye dhamana ya kuhakikisha nia njema ya Rais Samia inafikiwa hivyo wananchi msiwe na shaka kwamba jambo hili la zahanati sasa litapatiwa ufumbuzi, ” amesema Jacob
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Saada Mwaruka, amewaambia wananchi hao kuwa tayari ameingiza zahanati hiyo kwenye mpango wa vipaumbele vya Halmashauri ya Mbogwe kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo wameitengea zaidi ya Sh milioni 50 ili kuikamilisha na ianze kutoa huduma.
Aidha, amewaomba wananchi hao kuwa na imani na viongozi wa Wilaya ya Mbogwe ambao wanamuwakilisha Rais Samia na kwamba kwa namna yoyote ile zahanati hiyo iliyosubiriwa kwa zaidi ya miaka 18 sasa itapatiwa ufumbuzi kwa msukumo wa pamoja.
Comments are closed.