Kituo cha afya chageuka kichaka

RC ang'aka, Mganga Mkuu wenzake matatani

KATAVI: Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewasimamisha kazi baadhi ya watumishi Kituo cha Afya Ugalla kilichopo Kata ya Ugalla Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi.

Watumishi hao wamesimishwa leo Februari 16, 2024 ili kupisha uchunguzi kutokana uzembe walioufanya wa kukitelekeza kituo hicho baada ya kufanya ziara na kukuta hali isiyoridhisha katika kituo hicho ambacho kimejaa nyasi na kutopata majibu ya kuridhisha.

Waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Nsimbo, Ofisa manunuzi, Ofisa tarafa, Mtendaji wa Kata ya Ugalla, Mtendaji wa Kijiji na wengine watakaobainika kuhusika.

“Mmenileta hapa ili nipongeze kwamba mnafanya kazi nzuri? au mlitegemea hapa mimi nije nifanye nini? na sasa hivi mnasema tupe masaa sijui mangapi tufanye usafi, wanini? wananchi wanaokaa huku ndiyo wanapaswa wafanyiwe usafi sio usafi ufanywe kwa wajili yangu mimi,” amesema Mrindoko.

Aidha, amesema kuwa sio sawa na haikubaliki wananchi wanaoishi Kata ya Ugalla kukutana na nyasi katika kituo hicho cha afya kilichofanywa nyumba ya wadudu kama mchwa na wengine.

Mrindoko amesikitishwa na taarifa za fedha kiasi cha Sh milioni 500 za ujenzi wa mradi huo kuisha pasipo mradi kukamilika.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhan amesema hali hiyo imefanywa na baadhi ya watendaji wa eneo hilo huku akisema kuwa ujenzi wa mradi huo wa kituo cha afya Ugalla umesimama kwa takribani mwaka mzima kutokana na fedha za mradi huo kuisha kabla ya mradi kukamilika.

Habari Zifananazo

Back to top button