Kituo cha Dakawa chakidhi kuwa urithi wa taifa

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema kuwa eneo la Kituo cha Maendeleo Dakawa mkoani Morogoro, limekidhi vigezo vya kuwa urithi wa taifa.

Mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, kinachoratibiwa na wizara hiyo, Boniface Kadili alisema hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu kituo hicho cha Dakawa.

“Tayari tumefanya tathmini na kujiridhisha kuwa eneo hilo limekidhi vigezo vya kuwa urithi wa taifa. Hivyo basi, Wizara ya Utamaduni na Wizara ya Maliasili tupo katika hatua ya mwisho ya kulitangaza kwenye gazeti eneo la Dakawa kuwa urithi wa taifa,” alisema.

Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, eneo hilo litatangazwa rasmi kuwa urithi wa taifa na kulindwa kisheria. Naye Naibu Mkurugenzi wa kituo hicho, Godfrey Msimbe alisema kituo hicho kinapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa ili kukuza historia iliyopo kwa vizazi vya sasa na kesho.

“Mwaka 2021, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliomba Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutafuta maeneo yote yaliyotumika na wapigania uhuru na Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini na vyama vingine vya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kuyatambua na baadaye kuyatangaza ili yaje yatangazwe kama sehemu ya utalii na urithi wa taifa.

“Tunashukuru Wizara ya Utamaduni imefika, Wizara ya Maliasili pia wako kwenye mchakato wa mwisho wa kwenda kutangaza kituo hiki kama hifadhi ya taifa,” alisema.

Alisema kwa kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiye mmiliki wa eneo lile, alishauri mchakato huo wa taasisi nyingine kufanyika kwa haraka ili kuhifadhi vitu visiwe hatarini kupotea. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nondo alisema eneo hilo lina mahandaki na makaburi ya waliokuwa wapigania uhuru wa ANC.

“Makaburi hayo ni kumbukumbu muhimu katika historia ya ukombozi wa Afrika,” alisema.

Alisema tume zilizoundwa na makatibu wakuu wa wizara ya elimu waliopita na wa sasa zilifanya tathmini na kupendekeza namna bora ya kuendesha kituo hicho, kwa kuwa malengo ya kuanzishwa kwake ni tofauti na majukumu ya sasa.

Kwa maelezo ya Katibu Mkuu, Profesa Nondo, mapendekezo hayo yaliyotolewa hivi sasa yanafanyiwa kazi.

Habari Zifananazo

Back to top button