UJENZI wa mradi wa kituo cha mabasi Nyegezi jijini Mwanza ambao sasa umefikia asilimia 96 unatarajiwa kupaisha mapato ya Mkoa wa Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sekiete Yahaya alisema stendi hiyo inajengwa kwa gharama ya Sh 15, 885,589,063/- tayari Sh 11,751,506,153 zimeishatumika.
Yahaya alisema Mwanza kuwa, stendi hiyo iliyoanza kujengwa Oktoba 2020 ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 katika Ibara ya 17 (viii).
Alisema ilani inasisitiza kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka serikali kuu kwa kuongeza makusanyo ya ndani na hivyo kupunguza ruzuku ya washirika wa maendeleo kwenye bajeti ya serikali kuu.
Yahaya alisema mradi huo haukukamilika kwa wakati kutokana na changamoto zikiwemo za vifaa kutopatikana kwa wakati kutokana janga la Covid0 19.
Alisema mkandarasi anayejenga mradi huo aliomba kuongezewa muda hadi Septemba 18 mwaka huu na maombi yake yaliwasilishwa Machi mwaka huu na yako katika hatua za uamuzi.
“Lengo la mradi huu ni kuongeza mapato katika halmashauri yetu ili kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu” alisema Yahaya.
Alisema kituo hicho kinatarajiwa kuwa na eneo la maegesho ya mabasi 120 kwa mkupuo, maegesho ya magari madogo 80, maduka madogo 60 na maduka makubwa 14, sehemu tatu za abiria wanaosubiri mabasi, vyoo viwili vyenye matundu 20.
Yahaya alisema katika ghorofa ya kwanza kuna jengo la abiria, benki mbili, maeneo mawili ya mama lishe, vibanda 38 vya tiketi, maduka tisa, choo chenye matundu sita na katika ghorofa ya pili kuna maduka 35, benki mbili, duka kubwa, vyoo vinne vyenye matundu 37.
Alisema mradi huo utasaidia pia kukuza biashara zingine kutoka mikoa na nchi jirani.
Mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, Hamduni Mariseli alisema ujenzi wa kituo hicho cha mabasi una tija katika kukuza biashara kwa wananchi wa kawaida na kukuza mapato ya halmashauri hivyo kuiwezesha kutoa huduma za afya, elimu, miundombinu na nyingine katika jamiii.