Kituo cha utalii kuibadili Iringa

KITUO kikubwa cha kutoa taarifa za utalii za Ukanda wa Kusini mwa Tanzania kitakachojengwa kwa zaidi ya Sh bilioni 18 katika eneo la Kihesa Kilolo mjini Iringa, kinatarajia kuuboresha muonekano wa mji wa huo na kuvutia watalii wengi zaidi.

Akizindua maonesho ya Karibu Kusini katika eneo hilo leo, Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki alisema kituo hicho kitajengwa kupitia Mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

“Zabuni ya Ujenzi wa mradi huu imetangazwa Septemba 5, mwaka huu na Mkataba kwa ajili ya kuanza ujenzi unatarajiwa kusainiwa mwanzoni mwa Mwezi Novemba, mwaka huu ambapo ujenzi wa kituo hiki unatarajia kutumia muda wa miezi 12,” alisema.

Sambamba na kituo hicho, Kairuki alisema Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) watajenga kituo cha utafiti wa wanyamapori cha Kusini na kuanzisha bustani ya Wanyama katika eneo hili.

“Aidha, Chuo cha Uhifadhi wa Wanyamapori – MWEKA na Chuo cha Taifa cha Utalii vitaanzisha matawi kwa ajili ya kufundisha kada mbalimbali za masuala ya Utalii. Pia, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha – AICC kitajenga kumbi za mikutano zenye hadhi ya kimataifa katika eneo hili la Kihesa Kilolo,” alisema.

Akiwaomba wadau mbalimbali kuungana na serikali kutumia fursa za utalii zilizopo ili kuendelea kunufaika na sekta hiyo katika ukanda huo wa Kusini, Kairuki alisema hayo yote yanafanyika ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuendeleza na kukuza sekta ya utalii Kusini mwa nchi.

Alisema sekta ya utalii ni miongoni mwa nguzo muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi, kutokana na mchango wake katika pato la Taifa, fedha za kigeni, uwekezaji na ajira.

“Sekta hii huchangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni na takriban ajira milioni 1.5 za moja kwa moja,” alisema.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Sekta hii imevunja rekodi kwa kupata watalii 1,638,850 sawa na ongezeko la asilimia 45.

9 walioliingizia Taifa jumla ya Sh bilioni 522.

7 sawa na ongezeko la asilimia 80 ya watalii 1,123,130 walioliingizia taifa Sh bilioni 290.4 mwaka wa fedha 2021/2022.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alisema mikoa ya Kusini imebarikiwa kuwa na vivutio vingi na vya kipekee kama vile Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ambayo ni kubwa kuliko zote hapa nchini, na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mikumi, Udzungwa, Kitulo na Katavi.

Vivilevile alisema ukanda huo una mapori ya akiba kama vile Mpanga-Kipengere na Selous; maeneo ya fukwe ya Bahari ya Hindi yaliyoko Lindi na Mtwara pamoja na maeneo ya fukwe ya Ziwa Nyasa na Tanganyika.

Alitaja vivutio vingine kuwa ni maeneo ya hifadhi za misitu asilia kama vile Ziwa Ngosi na hifadhi ya asili Kilombero; maporomoko ya maji ya Kalambo ambayo ni marefu Afrika; maeneo ya kihistoria kama vile Kimondo, makumbusho ya Mkwawa, magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara; pamoja na utalii wa utamaduni kama vile mila na desturi.

Pamoja na kuwepo kwa vivutio hivyo, Waziri wa Maliasilia na Utalii alisema wizara inatambua kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya utalii katika mikoa ya Ukanda wa utalii Kusini.

Alisema changamoto hizo zinahusiana na hali ya miundombinu, kutokuwepo usafiri wa moja kwa moja wa ndege, uendelezaji mdogo wa vivutio na uhaba wa nyumba za malazi zenye hadhi ya kimataifa.

Katika kukabiliana na changamoto hizi alisema Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii katika ukanda.

Alizitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ukiwemo uwanja wa ndege wa Songwe Mbeya; kupanua uwanja wa ndege wa Iringa, kujenga na kupanua barabara za katikati ya miji wa Mbeya na ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Igawa Tunduma yenye urefu wa kilomita 218.

Mbali na kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Njombe Makete ili kuwawezesha watalii kufika kirahisi katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo na kujenga ngazi za kushuka chini kuelekea maporomoko ya Kalambo, Kairuki alisema serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Iringa kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

“Kutokana na jitihada hizi zinazofanywa na Serikali na kwa kuzingatia utajiri wa rasilimali za utalii zilizopo Kusini, wadau mna fursa kubwa ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali za utalii kama vile wakala wa biashara za utalii, kujenga kambi za kulala wageni, kujenga hoteli, kumbi za mikutano na maeneo ya michezo mbalimbali,” alisema.

Maonesho hayo yanayoratibiwa kwa pamoja na mikoa 10 ya Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Morogoro, Songwe, Rukwa na Katavi yamebeba kauli mbiu isemayo ‘Utalii Karibu Kusini, Muelekeo Mpya wa Uwekezaji’

Habari Zifananazo

Back to top button