Kituo kusaidia wasichana kujengwa

MKURUGENZI Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative, Rebecca Gyumi amesema katika Mpango Mkakati wa miaka mitano wanatarajia kujenga kituo cha kuwahifadhi na kusaidia wasichana na watoto ambao ni manusura wa ukatili wa jinsia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo leo Dar es Salaam, Gyumi amesema kwa sasa nchini kuna uhaba wa nyumba salama za kuishi wasichana au watoto wanaopitia ukatili wa jinsia hivyo, wameona ni vyema kujenga kituo hicho.

Amesema kuwa kituo hicho kitakuwa sehemu salama ambayo itatoa huduma za kisheria na kisaikolojia kwa manusura wa unyanyasaji wa kijinsia.

Advertisement

” Kwa sasa wasichana hawa hawana mahali salama pa kuishi hata kama haki itakuwa imetendeka…. wanaofanya vitendo vya ukatili hupata adhabu ya miaka 30 au zaidi jela lakini msichana huyu anakuwa hayuko kwenye mazingira salama,” amesema Gyumi.

Mbali na ujenzi wa kituo hicho, mkakati huo wa pili unalenga kufikia mikoa minne na kufanya kazi katika Kata nyingi zaidi ili kuleta tija na mabadiliko katika upiganiaji haki za msichana na mtoto wa kike nchini na kuimarisha nguvu ya  sauti zao na uongozi.

Amesema mikoa itakayofikiwa ni ya Tabora, Dodoma, Pwani na Dar es Salaam kutokana na kuwepo kwa vitendo vingi vya ukatili na katika kufikia malengo hayo, wanahitaji takribani Sh bilioni 14.

“Tunalenga kubadili tamaduni na mazoea yanayorudisha nyuma haki ya mtoto wa kike, kuongeza uchechemuzi wa sera na sheria ili mifumo isiyorasmi iimarishwe pamoja na kuimarisha taasisi yetu kwa kufikia wasichana 35,000 moja kwa moja na wasichana milioni moja kwa njia mbalimbali ifikapo 2027,” ameeleza Gyumi.

Pia ametaja mafanikio ya mkakati wa kwanza uliomalizika mwaka 2022, kwamba wamefanikiwa kuanzisha klabu za Amani zaidi ya 50 ambazo zimewafikia wasichana 3,000 na kwamba zimekuwa zikishughulikia  ukatili na kukuza usalama.

Amesema katika mradi wa Gape wamewezeaha wasichana 301 kiuchumi  pamoja na mradi wa baskeli kwa wasichana ambao umewezesha wasichana 500 kuendelea na masomo na wale waliopata mimba kurudi shuleni.

“Tumefanikiwa kuleta uchechemuzi katika sera na sheria hususan ya kubadilishwa kwa sheria ya ndoa za utotoni, mmeona kumekuwa na  vuguvugu nchini la kubadilishwa sheria ya ndoa, tunaamini litafanyiwa kazi,” amesisisitiza.

Katika mradi wa Msichana Kafee umewezesha kutungwa kwa sheria ndogondogo kwa ngazi ya Kata za kulinda haki za wasichana sambamba na kuratibu kesi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Msichana Initiative, Profesa Bertha Koda amesema serikali imefanya jitihada kubwa katika kuchangia shughuli zao na kutatua changamoto za wasichana ikiwemo kubadilisha mitaala ya elimu na kutunga sera inayoruhusu mwanafunzi aliyepata mimba kurudi shuleni.

“Changamoto zilizopo  ni pamoja  mimba na ndoa na ukeketaji, ulawiti na ubakaji. Pia   wasichana ni kundi kubwa linaathirika na Virusi Vya Ukimwi kwa kukosa afya ya uzazi hivyo,  tunahitaji kuongeza nguvu kufanya kazi kwa pamoja na kuchangia katika kufanikisha mpango mkakati wa miaka mitano,” amesema Profesa Koda.

 

6 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *