Kivuli cha Simba, Dodoma Vs Yanga

Nani kutinga Robo Fainali?

DODOMA: Vuta N’kuvute ya Kombe la Shirikisho la CRDB inaendelea leo kwa mchezo wa hatua ya 16 bora kupigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji FC dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Yanga.

Mchezo huo anatizamwa zaidi kutokana na Mashujaa FC jana kutuma salamu kwa vigogo wa Kariakoo Simba na kuiondosha katika michuano hiyo, hivyo leo Yanga anatizamwa ikiwa atakwepa jinamizi lililomkumba pacha wake Simba.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa ni Februari 05 mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Azam Complex na Yanga waliibuka washindi kwa bao 1-0, bao la Mudathiri Yahya dakika ya 86.

Kuelekea mchezo huo kocha wa Dodoma Jiji Francis Baraza amesema anaheshimu ubora walio nao wapinzani wake lakini hilo halihalalishi wao kufungwa kwenye mchezo huo wa leo usiku.

Ameongeza ni lazima wachezaji wake waepuke kufanya makosa kwani unapocheza na timu ya daraja la Yanga ukifanya makosa lazima uadhibiwe.

Nahodha msaidizi wa Yanga Dickson Job amesema wao kazi ni moja tuu kusaka ushindi ili kwenda katika hatua inayofuta ya Robo Fainali.

Hata hivyo Meneja wa Yanga Walter Harison amesema watawakosa wachezaji watatu Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Kouassi Attohoula Yao ambao wanatarajiwa kurejea kwenye michezo inayofuata.

Habari Zifananazo

Back to top button