MWEKEZAJI Jack Feng kutoka China anatarajia kuwekeza dola za Marekani zaidi ya milioni 311 (takribaniSh bil 725) katika mradi wa kuzalisha vioo katika Kijiji cha Mkiu Mkuranga, mkoani Pwani.
Jumapili, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), John Mnali, alisema ujenzi wa kiwanda hicho tayari upo katika hatua za awali ya utekelezaji.
Mnali alisema ujio wa kiwanda hicho utakuwa na manufaa kwa uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla.
Alisema thamani ya uwekezaji kwa mradi huo ni Dola za Marekani zaidi ya milioni 311 ambazo zitaimarisha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) katika uchumi.
Pia Mnali alisema mradi huo utasaidia kuchochea sekta nyingine kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya malighafi itatoka Tanzania.
“Nchi itapata fedha nyingi za kigeni kwa kuwa asilimia 70 hadi 80 ya bidhaa zitauzwa nje ya nchi katika masoko ya nchi jirani,” alisema.
Mnali alisema mradi huo pia utaongeza mapato ya fedha za kigeni kwa kuwa utaifanya Tanzania kupunguza uagizaji wa bidhaa za kioo kutoka nje na badala yake itauza bidhaa hizo nje ya nchi.
Alisema mradi huo utakuwa moja ya vyanzo muhimu katika kuchangia ukuaji wa pato la taifa, kuongeza ukuaji wa viwanda na shughuli za kiuchumi, uhamishaji wa teknolojia ya vioo kutoka nje kuja hapa n hini pamoja na Watanzania kupata ujuzi mpya.
Pia alisema mradi huo utachochea sekta ya madini na sekta ya huduma na asilimia 80 ya malighafi sawa na zaidi ya tani 300,000 za malighafi kwa mwaka zitapatikana ndani ya nchi ikiwemo mchanga, feldspar, dolomite na chokaa.
Feng alisema mradi huo ukikamilika, utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 700 kwa siku kwa hatua ya kwanza ya uzalishaji na tani 500 kwa siku katika hatua ya pili ya uzalishaji na wanatarajia kuzalisha ajira zaidi ya 1, 655 za moja kwa moja na ajira 6,000 zisizo za moja kwa moja.
Comments are closed.