Kiwango cha chini pensheni Sh 100,000

WASTAAFU wote wa Serikali wameboreshewa pensheni zao za kila mwezi, ambapo kiwango cha chini kwa sasa ni Sh 100,000, Bunge limeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Uemavu), Patrobas Katambi alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Nancy Nyalusi aliyetaka kujua ni lini serikali itaboresha mafao ya wastaafu kwa kuongeza kipato cha pensheni anayopata mstaafu kila mwezi.

“Mifuko ya Hifadhi ya Jamii huongeza kiwango cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu mara baada ya kufanya tathmini na kujua uendelevu wake na uwezo wa kulipa mafao kwa wanachama wake.

“Tathmini hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kipindi kifupi, miaka mitano kwa kipindi cha kati na tathmini ya kipindi kirefu ni miaka kumi.

“Mheshimiwa Spika, Kanuni za ulipaji mafao Namba 11(1) za mwaka 2018 zilielekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuongeza pensheni kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uendelevu wa Mfuko kila baada ya miaka mitatu.

“ Hata hivyo, ninayo furaha kuliarifu Bunge lako kuwa hadi sasa wastaafu wote wa Serikali walishaboreshewa pensheni zao za kila mwezi, ambapo kiwango cha chini ni Sh 100,000 na kuendelea tofauti na hapo awali,” amesema Naibu Waziri huyo.

Habari Zifananazo

Back to top button