Kiwango cha uchakataji gesi asilia chaongezeka

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kiwango cha uchakataji wa gesi asilia kwa miaka nane katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba mkoani hapa kimeongezeka kutoka futi za ujazo milioni 20 mwaka 2015 hadi kufikia futi za ujazo milioni 110 mwaka huu.

Aidha katika kipindi hicho kiwanda kimezalisha gesi zenye ujazo wa futi bilioni 14.714 huku wakizalisha gesi asilia ya kutosha na yenye ubora.

Meneja wa Kiwanda cha Madimba,  Leons Mrosso alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kutoka mkoani Dar es Salaam waliotembelea visima vya gesi vya Mnazi Bay na kiwanda hicho kujifunza namna gesi inavyozalishwa na kusafirishwa kwa matumizi mbalimbali.

Kiwanda cha Madimba kinamilikiwa na kampuni tanzu ya TPDC ya kusambaza gesi asilia (Gasco).

Alisema licha ya ongezeko la gesi kwa miaka hiyo, kiwanda kimekuwa kikisimamiwa na kufanya kazi na wazawa na kuendesha shughuli zote kitaalamu bila kupata changamoto yoyote hivyo kujivunia Watanzania kusimamia mradi huo mkubwa ambao ni wa kwanza katika kuchakata gesi asilia.

Mrosso alisema katika kuhakikisha usalama wamekuwa na kamera 18 zinazoonesha kila upande wa kiwanda lakini wakiwa na mitambo ya kisasa ya kuhakikisha usalama wa gesi asilia.

Alisema wamekuwa akifanya ukaguzi kila wiki kwa kifaa maalumu kinachotambua iwapo kuna gesi inavuja sehemu, huku kukiwa na mitambo inayobainisha ikiwa kuna mitambo inavuja.

Alisema kiwanda hicho kilichoanza uzalishaji wa gesi asilia mwaka 2015 kimekuwa kikipokea gesi asilia na kusafisha kisha kusafirisha kwa bomba lenye urefu wa kilometa 551 kwenda mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya aina mbalimbali.

Alitaja matumizi hayo kuwa ni pamoja mgari, majumbani na hata kuzalisha umeme ambapo Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) linatumia kuzalisha umeme kwa zaidi ya asilimia 60.

“Katika uzalishaji wa umeme hapa kiwandani, pia tunazalisha umeme wa megawati tatu lakini pia kuna umeme wa matumizi ya Mtwara yanafanyika kwa kutumia gesi asilia jambalo linalosaidia kuokoa fedha za nchi kwa kununua mafuta ya kuzalisha umeme na kutunza mazingira,” alisema.

Mrosso alisema katika uchakataji gesi wamekuwa wakisafisha kuhakikisha kuwa matumizi yanafanyika kwa gesi iliyo safi na kutoa maji, mafuta ghafi na gesi chafu kwa kusafishwa katika kiwanda cha Madimba na Somangafungu huku bomba lenyewe likisafishwa kila wakati ili kuondoa tope linaloganda.

“Hapa kiwandani pia tuna kisima ambacho tunazalisha maji kwa ajili ya matumizi ya kiwandani n ahata kwneye nyumba za wafanyakazi huku kila siku tukiwapatia wanakijiji wa Kijiji cha Madimba lita zaidi ya 60,000 kwa ajili ya atumizi ambapo wameanzisha mradi wa kuuza maji kwa maendeleo ya kijiji,” alisema.

Alibainisha kuwa maji hayo yamepimwa katika maabara kwa ajili ya matumizi majumbani na kuidhinishwa na wataalamu wa maji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Naye Msimamizi uzalishaji wa gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay kutoka kampuni ya Kimataifa ya Maurel & Prom ya utafutaji na uchimbaji wa rasilimali mafuta na gesi, Hussein Chitemo alisema katika eneo hilo wana visima vitano vyenye uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 110 kwa siku.

Alisema uzalishaji wa gesi asilia ulianza mwaka 2005 na wana leseni ya kuzalisha gesi hiyo mpaka mwaka 2031 na kubainisha kuwa gesi ipo ya kutosha kufikia muda huo huku tafiti mablimbali zikifanywa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button