Kiwanja cha michezo kujengwa Mwenge
MANISPAA ya Kinondoni Dar es Salaam imesema iko katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa kiwanja cha michezo eneo la Mwenge lengo likiwa ni kuhamasisha michezo kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.
Mkuu wa wilaya hiyo, Saad Mtambule amesema hayo Dar es Salaam na kuongeza kuwa ujenzi huo unatokana na kutekeleza amri ya Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ya kuhamasisha michezo.
Amesema ufanyaji wa michezo unasaidia kuepusha magonjwa yasiyoambukiza katika jamii ambayo yamekuwa yakitumia fedha nyingi za serikali kwa ajili ya matibabu.
” Michezo ni mazoezi ya viungo ambayo pia yanaepusha kuongezeka uzito, magonjwa kama ya shinikizo la damu na hata kisukari,” amesema na kuongeza kuwa kwa wilaya hiyo tayari Kuna vikundi vya mazoezi vipatavyo 62.
Amesema maelekezo ya Waziri Mkuu pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhamasisha michezo na pia kulinda na kutunza maeneo ya wazi yaweze kutumika kwa mazoezi na michezo pamoja na kuamgalia maeneo mengine.
Ametolea mfano kwa eneo la Mbweni kuwa Ina maeneo matano yanayoweza kutumika kwa michezo na kuwataka wananchi kuyatumia maeneo hayo Kwa kufanya mazoezi ya michezo na viungo pia.
Aidha amesema maeneo ya fukwe pia yanaweza kutumika kwa mazoezi na michezo Kwa kuwa wilaya hiyo ina kilomita 42 za fukwe.
“Zipo fukwe kama za Msasani,Kidimbwi,Kunduchi ambazo zinaweza kutumika liicha ya kwamba yapo baadhi ya maeneo yanayotiririsha maji machafu kutoka majumbani,” amesema na kuongeza kuwa upomradio unaotekelezwa kuondoa kero ya maji machafu.