MWANDISHI mkongwe mstaafu wa Magazeti ya Serikali ya Daily News na Sunday News, Charles Kizigha (72) amezikwa leo katika makaburi ya Kondo, Dar es Salaam.
Kizigha aliaga dunia Agosti 27 mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Mamia ya waombolezaji jana waliuaga mwili wa Kizigha nyumbani kwake Mbezi Beach –Africana na kulikuwa na mkesha.
Miongoni mwa viongozi waliofika nyumbani hapo ni Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson.
“Baba tunashukuru kwa maisha yako hapa duniani, sisi watoto wako tunasema asante Mungu kwani umetulea vyema na umetuachia urithi wa hekima na maarifa, pumzika kwa amani,” aliandika Dk Tulia katika kitabu cha maombolezo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe alisema Kizigha alikuwa mfano wa kuigwa na mwalimu kwa waandishi wachanga.
Mhariri Mtendaji wa zamani wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Isack Mruma alisema alifanya kazi na Kizigha kwa miaka mitatu Daily News 1980 hadi 1982 yeye (Mruma) akaenda masomoni Uingereza.
“Alinipokea Daily News na Mimi ndiyo mtu pekee ambaye nilikuwa natumia typewriter yake maana ilikuwa nyeti sana na alikubali kwa kuwa siku niliyoanza kazi sikuwa na typewriter. Alinifuata jamaa mmoja akaniambia humuogopi Kizigha wewe akikukuta hee, kweli alipokuja alifoka yakaisha,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chua Chua aliandika katika kitabu cha maombolezo ‘Nimepokea msiba huu kwa masikitiko makubwa sana, pole dada Angela Kizigha na familia yote. Mungu amweke mahali pema peponi’.
Aliyewahi kuwa Mhariri Mtendaji wa TSN, Gabriel Nderumaki aliandika ‘pumzika kwa amani kaka Charles’.
Mruma alisema Kizigha alikuwa akitibiwa muda mrefu katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na Agosti 19 mwaka huu alilazwa hospitalini hapo akiendelea na matibabu na Agosti 27 jioni alifariki dunia.
Leo mwili wa marehemu utapelekwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)-Usharika wa Mbezi Beach kwa ajili ya ibada ya mazishi. Kizigha ameacha mke, watoto watatu na wajukuu. Alizaliwa Oktoba 11 mwaka 1950.
Kizigha alikuwa gwiji wa habari za uchunguzi na pia amekuwa mtumishi wa muda mrefu katika magazeti hayo ya Daily News na Sunday News hadi alipostaafu mwaka 2010.