WAKAZI wawili wa Dar es Salaam, Ally Kibope (25), mkazi wa Keko Mwanga na Athumani Omary (40) anayeishi Ilala Bungoni wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuingilia miundombinu na kulisababishia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) hasara ya Sh 273,532,315.04
Akisoma hati ya mashitaka mbele ya Hakimu mwandamizi, Rhoda Ngimilanga, wakili wa serikali, Yusuf Abood alidai kuwa Julai 24 mwaka huu eneo la Banda la Ngozi, Chang’ombe Wilaya ya Temeke washtakiwa hao waliingilia miundombinu ya Tanesco kwa kukata nyaya mbili za umeme zilizokuwa zimefukiwa chini.
Katika shitaka la pili, Abood alidai kuwa baada ya kukata nyaya hizo huduma zililegalega na kuisababishia Tanesco hasara ya shilingi 273,532,315.04.
Washitakiwa walirudishwa rumande hadi Septemba 8, mwaka huu.