Kizimbani kwa kujifanya askari polisi

MKAZI wa Magomeni mkoani Dar es Salaam, Benson Petro (28) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo akikabiliwa na mashitaka mawili.

Benson alishtakiwa kwa kujitambulisha kwa mlalamikaji, Lightness Simon kama askari polisi pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh 200,000 kutoka kwa mlalamikaji huyo.

Akisoma hati ya mashitaka mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Claudis Kipande, karani Emmy Mwansasu alidai kuwa Aprili 20, mwaka huu majira ya saa 7:30 Mtaa wa Mkunguni katika Soko la Kisutu, mshitakiwa alijitambulisha kwa Lightness kama askari polisi huku akijua sio kweli na ni kosa kisheria.

Katika kosa la pili, Emmy alidai kuwa katika tarehe na eneo tajwa mshitakiwa alijipatia Sh 200,000 kutoka kwa Lightness kwa ahadi ya kumtafutia kazi huku akijua sio kweli.

Mshitakiwa alikana kutenda makosa yote aliyosomewa mahakamani hapo.

Kwa upande wake mlalamikaji ameieleza mahakama kuwa atakuwa na shahidi mmoja katika kesi hiyo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 24, mwaka huu itakaporudi tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa huku dhamana kwa mshitakiwa ikiwa wazi kwa sharti la kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh 200,000.

Habari Zifananazo

Back to top button