Kizimbani kwa kukata mtu sikio

DAR ES SALAAM: MFANYABIASHARA ,Kalumna George (18) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo akikabiliwa na mashtaka ya kumjeruhi mtu kwa kumkata sikio la kushoto.

George alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu, Gladness Njau kisha kusomewa mashtaka na karani wa mahakama hiyo, Caroline Nyonyi.

Nyonyi alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari Mosi, mwaka huu, katika eneo la Upanga Sea view barabara ya Obama katika Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.

Alidai mshtakiwa kwa makusudi alimjeruhi kwa kumkata na kisu sikio la kushoto, Yazidu Jafari na kumsababishia maumivu mwilini jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo, hivyo alirudishwa mahabusu hadi leo kwa ajili ya kesi yake kutajwa.

Wakati huo huo, Geofrey Njoele alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na mashtaka ya shambulio la kudhuru mwili.

Karani Nyonyi alidai kuwa mshtakiwa  alitenda kosa hilo Desemba 29, mwaka jana katika Mtaa wa Zanaki Wilaya ya IIala, Mkoa wa Dar es Salaam ambapo alimshambulia Ramadhani Bomani kwa kumpiga fimbo ya usoni upande wa juu ya jicho la kushoto.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo na aliachiwa kwa kujidhamini mwenyewe na kesi hiyo itatajwa Januari 8, mwaka huu.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button