KKKT kujenga Hospitali ya Rufaa Iringa

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa limepata ufadhili kutoka kwa marafiki zake wa Marekani na Ulaya utakaosaidia kuwawezesha kufanikisha azma yao ya kujenga hospitali kubwa ya rufaa katika eneo la Don Bosco Mkwawa, mjini Iringa.

Ujenzi wa mradi huo utakaokamilika ndani ya miaka minne unalenga kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha na kusogeza huduma za afya jirani na wananchi.

Akitoa taarifa hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa 13 wa sinodi uliofanyika mjini Iringa kwa siku nne, Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville, alisema  ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Advertisement

Alisema kujengwa kwa hospitali hiyo kutapunguza adha kubwa wanayoipata wananchi wa mkoa wa Iringa na maeneo yake jirani ya mlundikano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Askofu Gaville alisema pamoja na ujenzi wa hospitali hiyo, kanisa linaendelea na ujenzi wa seminari katika kijiji cha Ihemi wilayani Iringa unaotarajia kugharimu zaidi ya Sh Bilioni 2 hadi kukamilika kwake.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa KKKT,  Dk Fredrick Shoo ameishukuru na kuipongeza serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za kidini, ili nazo ziweze kutoa huduma zitakazoleta nafuu kwa wananchi.

Alisema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanikwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano kati ya taasisi za dini nchini, jambo ambalo limekuwa na tija katika kujenga taifa  lenye upendo, umoja na mshikamano.