Klabu ya gofu yapewa ekari 30 ujenzi wa kiwanja

HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa imeipa klabu ya gofu ya Mkwawa (Mkwawa Golf Club) ekari 30 katika eneo la utalii la Kihesa Kilolo mjini Iringa watakalolitumia kujenga viwanja tisa vya mchezo wa gofu pamoja na hoteli ya kitalii.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amezindua rasmi ujenzi wa viwanja hivyo katika hafla iliyohudhuriwa na wazee wa kimila na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Jesca Msambatavangu.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Edmund Mkwawa alisema wanahitaji zaidi ya Sh milioni 200 kukamilisha ujenzi wa viwanja hivyo ambao tayari umeanza pamoja na miundombinu yake mingine ikiwemo huduma ya maji.

Akiishukuru halmashauri kwa kuwapa eneo hilo, alisema gofu inaweza kuchangia kukuza utalii kwani mchezo huo huwawezesha watu kusafiri kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuucheza.

“Uwanja wa gofu unaweza kutumiwa kwa mikutano, mashindano, na matukio mbalimbali ya kijamii. Hii inaweza kuvutia watalii na wachezaji wa gofu kutoka maeneo mbalimbali,” alisema huku akiwaomba wadau kujitokeza kuchangia ujenzi wake.

Akizindua ujenzi wa viwanja hivyo, Mkuu wa Wilaya alisema serikali inatambua umuhimu wa michezo na kwamba ujenzi na uendeshaji wa uwanja wa gofu katika eneo hilo la utalii unaweza kutoa fursa za ajira kwa wenyeji na kuchochea uwekezaji katika sekta hiyo katika mikoa ya kusini.

Alisema watalii wanaokuja kucheza gofu wanaweza kuchangia katika uchumi wa ndani kwa kutumia fedha kwenye malazi, chakula, na shughuli nyingine za burudani.

Mbali na viwanja hivyo vya gofu Kessy alisema kituo kikubwa cha kutoa taarifa za utalii za ukanda wa kusini mwa Tanzania kitajengwa kwa zaidi ya Sh Bilioni 18 katika eneo hilo la Kihesa Kilolo.

Sambamba na kituo hicho Kairuki alisema Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) watajenga kituo cha utafiti wa wanyamapori cha Kusini na kuanzisha bustani ya Wanyama katika eneo hilo

“Aidha, Chuo cha Uhifadhi wa Wanyamapori – MWEKA na Chuo cha Taifa cha Utalii vitaanzisha matawi kwa ajili ya kufundisha kada mbalimbali za masuala ya Utalii. Pia, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha – AICC kitajenga kumbi za mikutano zenye hadhi ya kimataifa katika eneo hili la Kihesa Kilolo,” alisema.

Kwa upande wake mbunge wa Iringa Mjini, Dk Jesca Msambatavangu aliwaomba wadau mbalimbali kuungana na serikali kutumia fursa za utalii zilizopo ili kuendelea kunufaika na sekta hiyo katika ukanda huo wa Kusini.

Alisema sekta ya utalii ni miongoni mwa nguzo muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi, kutokana na mchango wake katika pato la Taifa, fedha za kigeni, uwekezaji na ajira.

Dk Msambatavangu alisema mikoa ya kusini imebarikiwa kuwa na vivutio vingi na vya kipekee kama vile Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ambayo ni kubwa kuliko zote hapa nchini, na hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mikumi, Udzungwa, Kitulo na Katavi.

Vivilevile alisema ukanda huo wa kusini una Mapori ya Akiba kama vile Mpanga-Kipengere na Selous; maeneo ya fukwe ya bahari ya Hindi yaliyoko Lindi na Mtwara pamoja na maeneo ya fukwe ya ziwa Nyasa na Tanganyika.

Alitaja vivutio vingine kuwa ni maeneo ya hifadhi za misitu asilia kama vile Ziwa Ngosi na hifadhi ya asili Kilombero; maporomoko ya maji ya Kalambo ambayo ni marefu Afrika; maeneo ya kihistoria kama vile Kimondo, makumbusho ya Mkwawa, magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara; pamoja na utalii wa utamaduni kama vile mila na desturi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x