Kocha alivyomficha Fabregas Barca wasimuone

SI ulishawahi kuusikia ule msemo wa Waswahili unaosema mbaya wako hatoki mbali, ndio ambao ulimtokea kiungo fundi raia wa Hispania, Francecs Fabregas ambaye mapema wiki hii ametangaza kutundika daluga.

Fabregas ambaye kwenye maisha yake yote ya soka la kulipwa amezichezea klabu tano tu ambazo ni Arsenal, Barcelona, Chelsea, AS Monaco pamoja na Como, amefikia uamuzi wa kuachana na kucheza soka akiwa na umri wa miaka 36.

Fabregas mpaka anastaafu hakutoka patupu, amefanikiwa kutwaa makombe yote ngazi ya klabu barani Ulaya na taifa isipokuwa moja tu ambalo ni Klabu Bingwa Ulaya (Uefa Champions League).

Ukirudi nyuma katika kupekua historia ya mchezaji huyu utakuta ikionesha FC Barcelona ndio waliokikuza kipaji chake kupitia kituo chao cha kukuza vipaji vya vijana cha La Masia.

Lakini kabla ya kufika kwenye kituo hicho alikumbana na kizingiti kizito ambacho kama si kufanikiwa kukiruka basi tusingekuwa tunamuongelea kama hivi sasa.

Fabregas alianza kuihisi harufu ya timu ya Barcelona tangu akiwa mdogo hajitambui, kwa mara ya kwanza kwenda uwanjani Barcelona ikicheza ilikuwa kipindi ana umri wa miezi nane ambapo babu yake ndiye alimchukua kwenda naye.

Safari yake ya soka ilianza kwenye timu ya watoto ya CE Mataro kisha kujiunga na watoto wa Barcelona halafu kwa wenzake Arsenal.

Akiwa Mataro ndipo alipokutana na changamoto ya kufichwa na kocha wake ili wasaka vipaji wasimuone wakamchukua. Inaelezwa kuwa Fabregas alikuwa ni mchezaji hatari sana tangu akiwa mdogo, wakati anajiunga na Mataro timu ambayo haikuwa kubwa na sio maarufu kwenye kukuza soka la vijana, kocha wake alijua wazi kuwa kuna wasaka vipaji kutoka timu kubwa lazima waje kumchukua na kwa nguvu ndogo za klabu yake asingeweza kumzuia.

Ili kuhakikisha mipango yake ya kuendelea kumbakiza kwenye kituo chake hicho akawa akimficha kutomchezesha kwenye baadhi ya mechi kubwa hasa dhidi ya Barcelona.

Aliendelea kumficha lakini ikafika muda akashindwa ikabidi amchezeshe ndipo Barcelona wakamuona na kumchukua. Kocha wake huyo aliwaruhusu Barcelona kumchukua ila kwa sharti kuu moja kuwa aende La Masia kufanya mazoezi mara moja tu kwa wiki.

Baada ya muda Mataro wakamuachia ajiunge na La Masia moja kwa moja huko alikutana na wachezaji wengi ambao wamefanya vizuri kwenye anga la soka akiwemo Lionel Messi na Gerard Pique.

Licha ya uhodari wake wa kufunga mabao 30 kwenye msimu mmoja katika ligi ya vijana, lakini alikosa nafasi ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza ndipo akatimkia Arsenal ambapo hakukaa sana kwenye kikosi cha vijana akapandishwa timu ya wakubwa na kuanza kuonesha makali yake.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button