Kocha Simba Queen akiri kuzidiwa

KOCHA wa Simba Queens, Charles Lukula amekiri kuwa Bayelsa Queens walikuwa bora kuliko timu yake na walistahili kushinda katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Prince Heritier Moulay El Hassan mjini Rabat, Morocco, ambao Simba Queens walifungwa 1-0, Lukalu alisema shambulizi pekee la Simba Queens lilifanywa dakika ya 70 lilipanguliwa na Wanigeria hao na kuyeyusha ndoto za kutwaa medali ya shaba.
“Wao (Bayelsa) Queens walituandama kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, labda wachezaji wangu wanasahau, kwa sababu ni kila dakika ya 70 ndipo tunapokosa kutumia nafasi tunazopata katika mechi tatu ni dakika hizo hizo,” alisema Lukula.
“Kwa baadhi yao, ilikuwa mara ya kwanza, ninafurahi kwani kufika hapa haikuwa rahisi, kwa sababu kila kitu kilikuwa kizuri. Bayelsa wanastahili ushindi kwa sababu wamekuwa wakicheza vizuri tangu mashindano haya yaanze. “Tulikuwa tunacheza dhidi ya timu bora pia, labda niseme, dakika 20 za kwanza tulikuwa na wasiwasi, lakini baada ya dakika 20, tulirudi mchezoni, kiukweli, tulicheza vizuri lakini labda hatukuleta matokeo zaidi kwa kuwaweka kwenye presha.”
“Unapocheza dhidi ya timu nzuri, hutarajii wasipate nafasi hivyo kwangu mchezo ulikuwa 50- 50 mtu yeyote anaweza kushinda, wasichana walicheza, ingawa labda, walimpa Bayelsa heshima kubwa,” aliendelea kusema.
“Nikirudi na kuangalia tatizo langu nitarudi na kutafuta washambuliaji wakali, hili ni eneo moja naharibu nafasi, hakuna mechi niliyocheza, na nisipate nafasi lakini washambuliaji wangu wana aibu.
“Wakati mwingine, wanacheza kitoto sana kwa sababu kuna wakati mwingine unahitaji kuua mchezo, unapopata mpira wako kutoka kwa mpinzani wako, kwamba katika mashindano makubwa, hutapata nafasi nyingi unapata mbili hadi tatu lakini ukifunga moja, unakuwa mzuri pamoja.
Hilo ni eneo moja ambalo tutalifanyia kazi. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), bingwa wa michuano hiyo ataondoka na dola za Marekani 400,000, mshindi wa pili dola 250,000 na timu zitakazocheza nusu fainali zitapata dola 200,000 kila mmoja.
Aidha, mshindi wa tatu atapata dola 150,000, wakati timu itakayoshika nafasi ya nne itapata dola 100,000.