Kocha wa Simbu afariki Dunia
Kocha wa mwanariadha maarufu wa Tanzania, Alphonce Simbu, Francis John amefariki Dunia.
John alifariki Dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya KMC Moshi baada ya kupata ajali Ijumàa usiku eneo la Maji ya Chai, Arusha wakitokea Dar es Salaam.
Katibu mkuu wa Chama Cha Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA), Rogat John alisema jana kuwa wanawasubiri ndugu wa marehemu kutoa ratiba na mpangilio wote wa mazishi ya kocha huyo wa Riadha.
Rogat alisema Francis alikuwa mwalimu wa kweli wa riadha na nyota wengine walipitia mikononi mwake.
Mbali na Simbu aliyeleta medali ya fedha katika Michezo ya Jumuiya ya Madola na medali ya shaba Mashindano ya Dunia, wengine walipitia mikononi mwake ni Christopher Isegwe. Mtanzania wa kwanza kushinda medali katika Mashindàno ya Dunia. Isegwe alitwaa medali ya fedha.
Wanariadha wengine walipitia mikononi mwa Kocha Francis na kutamba ni Samson Ramadhani mwenye medali ya dhahabu ya Jumuiya ya Madola, Bonay Akonay, Zebedayo Bayo na wengine.
Kocha huyo pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Riadha Tanzania (RT), kipindi ambacho Tanzania ikifanya vizuri sana katika Riadha kimataifa. Baada ya kumaliza kipindi chake, kocha Francis nafasi yake RT ilichukuliwa na Antony Mtaka.