“Kodi 2% imezingatia maoni kamati za wachimbaji”

MAMLAKA ya Mapato (TRA) imewatoa hofu wachimbaji wadogo mkoani Geita juu ya kodi ya asilimia mbili 2% ya mauzo itakayoanza kutozwa kwani mabadiliko yamezingatia maoni ya kamati za wachimbaji.

Ofisa kodi kutoka TRA Mkoa wa Geita, Sadick Rutenge ameeleza hayo wakati akizungumza na mashirikisho ya wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na madalali wa madini katika semina maalum mjini Geita.

Rutenge amesema mabadiliko ya sheria yanayofanywa na serikali katika sekta ya madini yanalenga kuongeza tija kwa kupunguza utitiri wa tozo na kuwatia motisha wachimbaji kulipa kodi hivo wayapokee.

“Nia na makusudi ya sheria hii, tuliweza kugundua kwamba kuna wachimbaji wengi ambao wanafanya biashara ya madini ambao kimsingi inakuwa ni ngumu kutunza kumbukumbu zao za uchimbaji.

“Kwa hiyo sheria hii imekuja kwa lengo la kuweza kumfanya mchimbaji mdogo atakapokuwa ameuza madini yake aweze kulipia hiyo asilimia mbili.

” Ameeleza na kuongeza;

“Sheria hii inawahusu wachimbaji wote ambao wanazalisha dhahabu kwa kutumia leseni ya awali (Primary Mining Licence) pamoja na wale ambao hawana leseni za uchimbaji (artisanal mining).

“Tumewaambia kabisa kwamba katika leseni walizonazo wenyewe ndio watakuwa wanakata ile asilimia mbili pamoja na kuilipa kwa serikali kwa sababu wao ndio wanunuzi ambao serikali imewaamini.”

Amebainisha, katika kufanikisha utekelezaji sheria hiyo, kwa kila soko la madini litakuwa na meneja wa TRA atakayewajibika kuhakikisha asilimia mbili inalipwa huku akiendelea kutoa elimu juu ya kodi hiyo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo mkoani Geita (GEREMA), Golden Hainga ameiomba TRA kuendelea kutoa elimu ya sheria hiyo mpya ili kuwajengea utamaduni wachimbaji kulipa kodi bila shinikizo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Wanawake mkoani Geita (GEWOMA), Asia Masimba ameiomba serikali kuendelea kuitikia punguzo la kodi kwenye biashara ya madini ili wajiendeshe kwa faida.

Habari Zifananazo

Back to top button