MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Maulida Anna Komu (73) ameieleza mahakama kuwa aliambiwa na chama hicho kuwa Halima Mdee na wenzake 18 waliandikiwa barua ya wito wa kufika Baraza Kuu lakini hawakwenda kwa kuhofia usalama wao.
Komu alidai hayo jana mbele ya Jaji Cyprian Mkeha wa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili watatu wabunge hao wa Viti Maalum, kutokana na kiapo kinzani alichokiwasilisha mahakamani hapo.
Mawakili hao ni Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge na Edson Kilatu, ambapo walimuuliza maswali mbalimbali ambayo yalikuwa yakihusiana na suala la Mdee na wenzake kutokupewa nafasi ya kusikilizwa na kisha kufukuzwa uanachama wao.
Panya: Chama kiliwaita kwa njia gani?
Komu: waliandikiwa barua ya wito lakini hawakufika kwasababu walisema ulinzi ulikuwa mdogo.
Panya: Halima na wenzake wanalalamika kuwa wamefukuzwa bila kuitwa?
Komu: Wao hawakutaka kusikilizwa, waliitwa na hawakwenda kwasababu ukikosana na mtu na akikuita lazima uende Ili msuluhishane sasa wao waliitwa ila hawakwenda.
Panya: umesema waliitwa na walikataa kwenda kwasababu ya kuhofia usalama wao je wewe unaona suala la usalama wao ni dogo?
Komu: si dogo kama ni kweli.
Panya: utaratibu wa kuendesha mashauri kwenye chama chako ukoje kwasababu wanalalamikaji wanasema chama kiliburuza demokrasia na hakikufuata taratibu za kushughulikia makosa ya viongozi?
Komu: kwakuwa mimi si mzoefu wa kusoma katiba sijui kama taratibu zilivunjwa na pia sifahamu kama walienda wakaonewa.
Panya: Halima na wenzake wanadai waliomba wapewe siku saba Ili walete utetezi wao kwasababu kilikuwa na shida ya usalama wao.
Komu: Sina habari kama waliomba au kuleta barua ya kuomba hizo siku saba.
Panya: Je unawatambua waleta maombi kama walikuwa viongozi wa chako?
Komu: Natambua.
Panya: Je ulishiriki kikao kilichofanyika Mei 11, 2022 kama mjumbe wa Baraza kuu?
Komu: hata sikuwepo kabisa kwasababu Mimi sio mjumbe wa Baraza kuu.
Kilatu: hapa mahakamani kuna kiapo kizani kinachoonesha kimesainiwa na wajumbe saba ikiwemo wew, je unakitambua?
Komu: ndio nakitambua
Kilatu: uliapa mambo iliyokuwa unayajua kweli au si kweli?
Komu: kweli
Kilatu: kwenye kiapo chako umesema waleta maombi waliitwa na hawakwenda pia umesema walishirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufoji barua ya kuwa wabunge lakini hapo awali umeiambia mahakama hukuwepo kwenye kikao cha Baraza kuu je hizi taarifa ulizitoa wapi?
Komu: nilizipata baada ya kusoma kiapo kizani ambacho sikuandika mimi na kuhusu kwamba hawakwenda niliambiwa walipewa nafasi ya kujitetea na hawakwenda kwahiyo nisome alafu niweke sahihi.
Kilatu: kwenye kiapo kizani kuna sehemu unawatuhumu Halima na wenzake kuwa walijiteua kuwa wabunge habari hizo ulizitoa wapi wakati ulikuwa ushiriki vikao vya Baraza kuu?
Komu: nilielezwa nilipoenda ofisini kwa Katibu wa Chama kwasababu kama unataka kujua taarifa za chama unazipata kwa Katibu.
Kilatu: Hadi sasa chama kina wabunge wangapi?.
Komu:Mmoja.
Kilatu: unaifahamu hoteli ya Ledger Palza
Komu: sipajui.
Kilatu:kama hupajui mbona kwenye kiapo kizani ulisema hali ya usalama wake ilikuwa ni salama na ipo shwari?
Komu sijui hali ya usalama kwasababu sihijuhi hiyo hoteli.
Kilatu: Novemba 26 na 27, 2020 Halima na wenzake walikuwa wapi?
Komu: sifahamu
Kilatu: wao wanasema walikuwa Dodoma wewe unasemaje?
Komu: sijui
Kilatu: chadema inatambua matumizi ya tehama?
Komu: inatambua
Kilatu: kama inatambua hawa 19 walipewa utaratibu wa kusikilizwa kwa njia ya mtandao?
Komu: sijui
Kilatu: walilalamika Novemba 11, 2022 ilitakiwa ifanyike kura ya siri na badala yake zilipigwa kura za wazi jambo lilifanya wajumbe wasiwe huru kutenda haki?
Komu: kwa kweli sijuhi.
Kilatu: moja ya malalamiko ni kwamba John Mnyika na Freeman Mbowe kuingia katika kwenye kikao cha kamati kuu na wakati walipoenda kukata rufaa wakawakuta hao hao kwenye Baraza kuu hivyo ni kinyume cha sheria na kanuni ya chama chenu, wew unasemaje?
Aliko: unamfahamu kama kuna taratibu za mtu kuvuliwa ubunge?
Komu: ndio zipo taratibu
Aliko : kama Tume ilishawatamka kuwa wabunge je chama kilifuata taratibu za kupinga wasiwe wabunge?
Komu: ndio kwakuwa chama hakiwatambui.
Aliko: hawa 19 kamati kuu iliwavua ubunge au uanachama?
Komu: iliwavua uanachama.
Mbali na Komu shahidi mwingine aliyehojiwa jana katika shauri hilo ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Francis Mushi (80) ambaye hata hivyo akumalizia kutoa ushahidi wake kwasababu ya muda.
Jaji Mkeha aliaharisha shauri hilo hadi Septemba 7 ,2023 saa tatu asubuhi ambapo, jopo la mawakili hao, litaendelea kumuhoji mjumbe wa bodi hiyo, Mushi.
Mdee na wenzake walifungua shauri hilo namba 36/2022 Julai 22, 2022 wakiomba Mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kisha itoe amri tatu.
Katika shauri hilo, wabunge hao wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama na pia iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza.
Comments are closed.