TAASIS ya wanawake Lakimoja imepanga kuwafikia wanawake nchini na kuwaelimisha kuhusu fursa ambazo hawajazifikia, lengo likiwa ni kukuza uchumi wao na nchi kwa ujumla.
Mshauri wa masuala ya utalii na uchumi kutoka taasisi hiyo, Dk There’s Mugodi, amesema hayo leo Dar es Salaam, wakati akizungungumza kuhusu kuwepo kwa kongamano lenye kuwakutanisha wanawake mbalimbali nchini Oktoba 15,2022.
Amesema kupitia kongamano hilo watawafikia wanawake walio wengi nchini, kuweza kuelimishwa namna wanavyoweza kuzitumia fursa hizo za utalii wa ndani na kukuza uchumi na kutangaza utalii nchini pia.
” Tunataka kupitia wanawake, kampuni za simu nchini kuja na ujumbe mfupi wenye kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, hatua ambayo itawezesha wanawake kushiriki na kujielimisha pia,” amesema Dk Mugodi na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia wanawake kujikomboa.
Amesema upo utalii wa maji chini ya bahari, ambapo inatakiwa kuwepo picha za chini ya ardhi, ambazo zitaongeza wigo wa watalii wanaoingia nchini, lakini pia kuwasaidia wanawake kiuchumi.
Amesema kupitia kongamano hilo, watabainisha ni fursa zipi wanawake wanaweza kuzifikia, ikiwemo pia kupika chakula cha kiutamaduni kulingana na makabila yao, suala ambalo litavutia watalii kwa namna moja hadi nyingine.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Nangasu Warema, amesema ipo haja ya kuelimishwa pia ya kuwepo kwa uwiano wa fursa za kitalii kijinsia, ili wanawaeke waweze kushiriki.
Amesema watahamasisha wanawake kujiunga katika makundi, lakini pia wataomba benki nchini kusaidia wanawake wajasiriamali, ili kuimarisha uchumi wao.
Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Veronica Nicholas amesema kupitia kongamano hilo, atasaidia wanawake kupambana na vitendo vya kikatili na kunyanyasika na hata vitendo hivyo kupungua pia.