Kongamano la watafiti, wanasayansi, wabunifu lilivyonoga Dar

“MCHANGO wa bioteknolojia ya kisasa katika kuendeza mapinduzi ya nne ya viwanda,” hiyo ni miongoni mwa mada zilizotikisa katika Kongamano na Maonesho ya Nane la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu lililoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia lililofanyika mkoani Dar es Salaam.

Kongamano hilo liliwakutanisha watafiti, wanasayansi, wabunifu na wanazuoni kwa ajili ya kupokea na kujadili matokeo ya shughuli za kisayansi, teknolojia na ubunifu nchini.

Katika kongamano hilo, Mhadhiri na Mtafiti katika eneo la bioteknolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Ally Mahadhy ameeleza kuwa kama nchi imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ongezeko kubwa la watu.

Advertisement

Hili linadhihirika kwa kuwa mwaka 2012 Tanzania kulikuwa na watu karibu milioni 45, lakini sensa iliyomalizika ya mwaka jana idadi ya watu ilikuwa karibu milioni 62.

“Wakati tukiendelea kuongezeka ardhi yetu inapungua sababu tunahitaji kupata maeneo ya kujenga na kufanya shughuli nyingine za kijamii.

“Wataalamu wanafanya makadirio kuwa ikifika mwaka 2030 pamoja na kwamba tumeongezeka sana, asilimia 60 ya watu watakuwa wanaishi mijini, watakaokuwa wamebakia vijijini kufanya shughuli za uzalishaji ni asilimia 40 tu,” anasema.

Hali hiyo inaonesha ni jinsi gani kama taifa litakavyoukabiliwa na changamoto, ikiwa jamii itabaki kwenye teknolojia inayozitumia.

Anasema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha maeneo yaliyokuwa yakipata mvua za kawaida hivi sasa yanakuwa na ukame, mafuriko na mvua zisizotabirika.

“Lakini maingiliano yetu na viumbe vingine vinasababisha kutokea kwa vimelea vya maradhi vipya, zamani vilikuwa vinaishia kwa wanyama sasa vinakuja mpaka kwa binadamu.

“Zote hizi zinachangia katika uwepo wa ukosefu wa chakula au tuseme matatizo katika sekta ya chakula, usalama, lakini pia uhifadhi wa chakula,” anasema.

Dk Mahadhy anasema binadamu ameonesha historia yuko mpaka sasa kwa sababu ana uwezo wa kukabiliana na changamoto zake kwa kujaribu kuja na masuluhisho ya matatizo yake, ili aendelee kuwepo.

Kwa mujibu wa Dk Mahadhy bioteknolojia ni moja kati ya sehemu muhimu katika mapinduzi haya ya nne ya viwanda.

Bioteknolojia ni nini?

Bioteknolojia ni matumizi ya viumbe hai kwa ajili ya kuzalisha mazao mbalimbali, lakini pia kwa ajili ya kutengeneza mifumo itakayowezesha kutatua matatizo.

“Kwa mfano kwa mkemia mkuu kama unataka kujua mtoto ni wako au si wako, kwa kutumia sehemu ya viumbe hai cha kwako vinaitwa vinasaba kuna mifumo imetengenezwa wanaweza kukuambia huyo mtoto ni wako au la,” anasema.

Na moja kati ya bioteknolojia maarufu, lakini haiko peke yake ni ni biotekinolojia ya uhandisi jeni (GMO).

“Kwenye kilimo bioteknolojia kwenye uhifadhi wa chakula tunazalisha mbegu mbalimbali ambazo zinastahimili maradhi. Mfano mgomba unaostahimili ugonjwa wa mnyauko maarufu kama ukimwi wa migomba.

“Huyo bakteria anashambulia migomba yote kwa hiyo wanasayansi wakagundua kuwa pilipili hoho haishambuliwi na huyo bakteria, kwa hiyo wakahamisha taarifa wakaweka kwenye mgomba ukawa na uwezo wa kustahimili hayo magonjwa hii imefanyika Uganda,” anasema.

Lakini pia anaelezea mimea inayojikinga na wadudu waharibifu na kutolea mfano wa mahindi yanayostahimili wadudu utafiti ambao umefanyika nchini Kenya, ambao kwa sasa wanazalisha miche, ili sheria yao ikikaa vizuri wawe na miche ya kutosha.

Pia anazungumzia mimea inayostahimili ukame iliyofanyiwa utafiti hapa Tanzania katika eneo la Makutupora mkoani Dodoma.

“Tuiangalie teknolojia na faida zake na kama kuna changamoto kama ambavyo teknolojia nyingine moto ukipikia unaweza kukuunguza tuweke mifumo ya kuhakikisha tunapata zile faida na kuepuka na hasara,”anasema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu ameelezea lengo la kongamano la kisayansi lililofanyika Juni 14 mpaka 16 mwaka huu mkoani Dar es Salaam ni kuwaweka  pamoja watafiti, wanazuoni, wabunifu na wagunduzi, watunga sera na wafanya maamuzi, ili kubadilishana uzoefu kuhusu namna sayansi, teknolojia na ubunifu unavyoweza kuchangia katika ukuaji wa kiuchumi wa Taifa na kufanikisha mpango wa maendeleo wa Taifa 2025.

Anakumbusha kuwa Sheria Na. 7 ya Bunge ya mwaka 1986, imeipa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia jukumu la kuwa mshauri mkuu wa Serikali katika masuala yote yanayohusu sayansi, teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya taifa.

Ikiwa ni pamoja na kuratibu, kukuza na kuendeleza utafiti vile vile kuratibu, kuendeleza na kuhawilisha teknolojia na ubunifu, kukusanya, kuhifadhi na kusambaza taarifa za sayansi, teknolojia na ubunifu ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha kutoka serikalini na wadau wengine kwa ajili ya kukuza na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu.

“Kukuza mahusiano ya kikanda na kimataifa katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu; na kushauri serikali kuhusu masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yakiwemo vipaumbele vya utafiti, mgawo wa matumizi ya fedha za utafiti kufuatana na vipaumbele vilivyokubaliwa, ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika utafiti, mafunzo na ajira za watafiti, na Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia.

“Tume inasimamia mfumo mzima wa sayansi, teknolojia na ubunifu, ili uweze kutoa mchango wake kijamii na kiuchumi hapa nchini,” anasema.

Anasema Tume imewezesha watafiti wa ndani na nje ya nchi kufanya tafiti hapa nchini kwa kuratibu utoaji wa vibali vya utafiti. Katika baadhi ya maombi ya vibali vya tafiti, Tume hushirikisha wadau wa sekta husika ili wafahamu utafiti gani unaendelea, wajiandae kupokea matokeo ya tafiti hizo yaweze kutumika na serikali.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda kwenye kongamano hilo la sayansi ambalo aliwakilishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Profesa Lugano Kusiluka, ametaja kauli mbiu ya kongamano hilo kuwa ni Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Maendeleo Endelelevu.

“Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 na 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Miaka mitano 2021/22 mpaka 2025/26 vinasisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo endelevu nchini.

“Hiyo ikijumisha ugunduzi wa mbegu na miche bora, matumizi ua sayansi, teknolojia na ubunifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ujenzi wa uchumi imara na endelevu kwa nchi,” amesema.

Mwaka jana katika uzinduzi wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (BST), Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tnzania (TARI), Kituo cha Mikocheni mkoani Dar es Salaam, Fred Tairo alisema bioteknolojia ina mchango mkubwa katika kuchangia upatikanaji wa chakula na lishe.

Usalama wa chakula na lishe, ubora wa maisha, mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa mazingira.

Alishauri kuwa ni muhimu kuimarisha uwezo wa wa matumizi ya teknolojia kwa fedha na wataalam wa miundombinu na kushauri ni muhimu kuendelea kuinua uelewa na maarifa ya umma juu ya baiteknolojia.

Naye Dk Traore Edgar wa Burkina Faso anasema anaiona teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) kama tekinolojia nyingine ya uboreshaji maisha ya binadamu.

“Ni vyepesi sana kutuma jumbe , sauti na picha kwa kutumia simu janja za androidi tofauti na hapo baadaye tulipokuwa tunatuma jumbe kwa posta, Ni sawa? Kwa ujumla watu wanapokea vizuri mabadiliko ya teknolojia.

“Hata hivyo bado kuna wasiwasi kwenye tekinolojia ya GMO. Kiuhalisia, siyo sahihi kuiongelea GMO kwa ujumla wake, badala yake inatakiwa kung’amua na kuiongelea tekinolojia moja wapo,” amesema.

Barani Afrika anasema teknolojia hiyo imeleta mapinduzi ya kilimo katika nchi ya Afrika ya kusini , Sudani , Burkina Faso na Nigeria.

“Kwa kutumia teknolojia hii mbegu zinaweza kutengeneza kinga yake dhidi wadudu hivyo kutoa suluhu kwa njia ya kawaida ambayo ingheitaji nguvu kazi kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Anasema Hata hivyo GMO bado inaogopeka Afrika kutokana na mijadala pinzani inayoendelea dhidi  yake.

Ushauri wake ni kwamba Afrika, baada ya kuyakosa mapinduzi ya kijani ya kiulimwengu inanafasi ya kuhodhi tekinolojia za kibunifu kama hizo ili ijitosheleze kwa kuwa na chakula cha kutosha.

Tofauti na hivyo, nchi nyingine duniani watatakiwa waje kwa mwanvuli wa misaada ya chakula ambayo itakuwa na GMO ambayo tunasita kuitumia.

 

1 comments

Comments are closed.