Kongwa wampa ‘tano’ Rais Samia miradi ya maendeleo

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa  mkoani Dodoma limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia halmashauri hiyo fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Pongezi hizo zimetolewa katika baraza la madiwani lililoketi mwishoni mwa wiki kujadili taarifa za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022.

Akitoa hotuba mbele ya baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, White Zuberi alimshukuru Rais Samia  kwa uongozi wake imara na kuongeza kuwa licha ya changamoto zinazolikabili taifa, lakini usalama pamoja na majukumu ya kitaifa, vimeendelea kuimarishwa.

“Kazi ya urais siyo kazi ndogo, ndiyo kazi ya mwisho ya uongozi katika nchi. Anaongoza watanzania zaidi ya milioni 60. Lakini pamoja na changamoto zote za nchi, bado nchi inaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida,” alisema.

Aidha Zuberi  ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuchangia maendeleo kupitia tozo za miamala kwa kuwa fedha hizo zinatumika kwenye ujenzi wa miradi, hivyo amewataka madiwani kuhakikisha wanawaeleza wananchi kuhusu faida za tozo.

“Ni kweli ni ngumu sana kujichangisha, wengi tunapenda tupewe, tutapewa mpaka lini? ni lazima na sisi kama watanzania tuchangie maendeleo yetu,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri  hiyo, Richard Mwite, ameiomba serikali kuendelea kuipatia halmashauri fedha za tozo  kwa mara nyingine kwa kuwa inao uwezo wa kuzisimamia, ikizingatiwa kuwa hali ya makusanyo kwa kipindi cha robo ya nne, halmashauri ilivuka lengo.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi(VVU) kwa kuwa ugonjwa huo bado ni tishio.

Alibainisha kuwa kwa kipindi cha Aprili  hadi Juni, 2022,  kati ya watu 4,693 waliopimwa kwa hiari, 79 walikutwa na maambukizi ya VVU ambao ni sawa na asilimia  4.2.

Mwite alihamasisha wananchi kuendelea kujitokeza  kupata chanjo ya Covid- 19, kwa kuwa chanjo hiyo ni muhimu kwa afya zao.

Akizungumzia suala la utoro shuleni,  Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dk Omary Nkullo ameliambia baraza hilo  kuwa imeanzishwa Oparesheni maalumu ya futa utoro ambapo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi uongozi utapita katika maeneo mbalimbali kuwakamata wazazi walioshindikana na kuwafungulia kesi.

“Tumekubaliana jana(juzi) kwamba wale ambao itashindikana kabisa basi OCD(Mkuu wa Polisi wa wilaya) tutakuomba nguvu yako, tutakuwekea mafuta kwenye gari yako, tuzunguke kijiji kimoja baada ya kingine tukamate wale wazazi walioshindikana,” alisema.

Wilaya ya Kongwa ni miongoni mwa halmashauri zilizonufaika na miradi iliyotokana na fedha za tozo ya miamala ya simu.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button