TAASISI ya kimataifa ya Afya nchini Korea (KOFIH), imetoa jumla ya Dola za Marekani milioni tano (sawa na Sh 2,391,000,000) kwa ajili ya awamu ya pili ya mradi wa mapambano dhidi ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga katika halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani.
Hayo yalibainishwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Subira Mumba wakati wa mkutano kutathmini miaka saba ya awamu ya kwanza ya mradi huo, uliofanyika katika ukumbi wa shule ya kimataifa ya uongozi ya Julius Nyerere, mjini Kibaha.
Alisema fedha hizo ambazo zimetolewa kwa ufadhili wa taasisi hiyo, utadumu kwa miaka mitano na umelenga kuwafikia wanawake wote wajawazito, watoto wachanga wa Mkoa wa Pwani kupitia halmashauri tisa.
“Baada ya kumaliza awamu ya kwanza ya mradi huu, tunaishukuru taasisi ya KOFIH kwa kukubali tena kutoa fedha zaidi ya Dola milioni tano za Marekani ambapo kwa sasa wanawake na watoto wachanga wote wa Mkoa wa Pwani watanufaika,” alisema.
Alisema awamu ya kwanza ya mradi huo, ulizinufaisha halmashauri za wilaya sita ambapo uliwezesha kununuliwa kwa magari matano ya kubebea wagonjwa, kujengwa wodi za wazazi, ujenzi wa vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya.
Subira alisema mradi wa awamu ya kwanza ulianza mwaka 2016 na kwamba umefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka watoto zaidi ya 800 na kufikia watoto 335 wakati vifo vya wanawake vikipungua kutoka vifo 88 hadi vifo 35.
Awali akizungumza katika mkutano huo kwa njia ya mtandao, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya mama na mtoto wa Wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani alisema mradi wa kwanza uligaharimu jumla ya Sh bilioni 9.5.
“Mradi huo wa awamu ya kwanza ulivifikia vituo vya afya 19 katika wilaya sita ambazo ni Kihaba Mjini, Kibaha Vijijini, Rufiji, Kibiti na Mafia na lilijengwa jengo la wazazi, vyumba vya upasuaji na vifaa tiba,” alisema.