Korosho Marathon kufanyika Septemba 2 Mtwara
MSIMU wa pili wa mbio za Korosho Marathon utafanyika Septemba 2, 2023 katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Akizungumzia mbio hizo leo mkoani humo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred amesema mbio hizo ni za hisani kama ilivyokuwa mbio zingine zinazotokana na juhudi za serikali kupitia bodi hiyo zenye lengo la kuwezesha maendeleo ya tasnia hiyo kwa kuhamasisha uzalishaji, usindikaji, ulaji wa korosho.
Hata hivyo kujitangaza katika kuhimiza wadau hasa Wananchi kuongeza matumizi hayo ya ulaji wa bidhaa hiyo na matumizi ya mazao ya korosho kama vile maziwa, juisi, mafuta ya kula ambapo fedha zitakazopatikana na mbio hizo zitakwenda kuwezesha vikundi mbalimbali vya ubanguaji wa korosho ikiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwenye mikoa inayolima zao hilo.
Aidha, kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa tasnia ya zao hilo nchini hasa ubanguaji, kuchangia katika utatuzi wa changamoto zilizopo katika sekta ya elimu kwa kununua madawati yatakayo gawiwa kwenye shule za msingi mikoa ya Lindi na Mtwara.
‘’Bodi ya korosho inaamini wananchi wakitumia korosho kwa wingi itahamasisha kuongezeka kwa ubanguaji wa ndani, kuongeza thamani ya korosho kwa kupata bei nzuri na hatimaye kuwa na soko la uhakika hivyo naomba kuihamasisha jamii kujitokeza na kujisajili ili kushiriki mbio hizi ili tuje tufurahi, tujenge afya huku tukichangia maendeleo ya elimu na ukuaji wa soko la korosho nchini’’, amesema Alfred.
Katibu wa mbio hizo, Mhandisi Sebastian Kiyoyo amesema mbio zitakuwa za umbali wa kilomita 21, 5, 10 na washindi wa mbio hizo wa kwanza mpaka 10 wote watapata zawadi huku mshindi wa kilometa 21 atapata Sh milioni 4 ambapo mpaka sasa idadi ya washiriki inaendelea kuongezeka na gharama za ushiriki Sh 30,000 huku matarajio yao ni kupata washiriki 1500.
Mwenyekiti wa uhamasishaji wa mbio hizo, Mohamed Kemkem ameongeza kuwa hamasa za mbio hizo zitachagizwa na mwanamuziki wa Bongo Fleva Nassibu Abdul “Diamond Planum” huku akitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo mengine nchini kutumia fursa hiyo kufanya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.